Na. Stanley Brayton, WMUV
Longido
Julai 20, 2025
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede, amezitaka Taasisi zinazofanya kazi katika mpaka wa Namanga kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta tija katika Uzalishaji na kutekeleza majukumu yao na kuleta matokeo chanya.
Akizungumza leo Julai 20, 2025 alipotembelea Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP), Mnada wa Upili na Idara ya Huduma za Mifugo vilivyoko katika mpaka wa Namanga, Wilaya ya Longido, kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa shughuli za Uvuvi na Mifugo katika eneo hilo na kuongea na Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walioko katika Kituo hicho ili kubaini changamoto zinazowakabaili maafisa katika kutekeleza majukumu yao, Dkt. Mhede amesema ni muhimu kushirikiana kati ya Taasisi na Taasisi katika kuleta tija na kuongeza uzalishaji pamoja na Maendeleo nchini.
Vilevile, Dkt. Mhede amesema ni vyema Wataalam wa Sekta zote kushirikiana na wadau kwa kukaa nao vikao vya pamoja ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Aidha, Dkt. Mhede ameelekeza Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kufanya maandalizi kwa ajili ya kupandikiza vifaranga vya samaki katika Mabwawa ya Manyara, Eda Chini na Eyasi ili kuongeza Uzalishaji wa zao hilo la Samaki katika Mabwawa hayo na kuleta tija katika Sekta hiyo.
Pia, Dkt. Mhede, amitaka Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kufuatilia Mabwawa ya asili ambayo yapo Mikoani, hususani katika Mkoa wa Arusha na Manyara kwa ajili ya kupandikiza vifaranga ili kuongeza uzalishaji nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni