Na. Stanley Brayton, WMUV
Kibaha, Pwani
Julai 30, 2025
⬛ Ataka Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala na Kampuni ya NARCO kuweka alama kwenye mipaka ya maeneo yao.
⬛ Ataka Dawati la Ndege Wafugwao kuanzisha Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ya Kuku
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amewataka Wafugaji na Wafanyabiashara za Mifugo kupeleka Mifugo yao kwenye kituo cha Karantini ya Mifugo ili kufanyiwa Uchunguzi wa Magonjwa kabla ya kuuza Mifugo hiyo nchi za nje, ikiwa ni njia moja wapo ya kukuza Biashara hiyo Kimataifa.
Akizungumza wakati alipotembelea Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Shamba la Kuku la Kampuni ya Tanzania Sunshine na Kampuni ya Mkuza Chicks, leo Julai 30, 2025 Mkoani Pwani, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amesema uwepo wa Kituo cha Karantini ya Mifugo ni fursa ya kimkakati katika kuyafikia masoko ya mifugo na mazao yake ya ndani na nje ya nchi.
“Kituo hiki ni muhimu sana, na kimekaa Kimkakati, hivyo kinatakiwa kifanye kazi ipasavyo ili wafugaji waone umuhimu wake na kuweza kunufaika nacho Kibiashara, kwani kinasaidia kuwahakikishia usalama wa mifugo na mazao yake hasa katika Masoko ya nje ya nchi.” amesema Bi. Meena
Aidha, Bi. Meena ameitaka Idara ya Huduma za Mifugo kuweka utaratibu wa kila Mfugaji au Mfanyabiashara ya Mifugo kupitisha Mifugo yao katika karantini kabla ya kwenda kuuza nje ya nchi, na ameielekeza idara kuangalia namna bora ya kuboresha Miundombinu ya Kituo hicho ili kiweze kutoa huduma Bora zaidi.
Vilevile, Bi. Meena amesisitiza kuwa Karantini ina maslahi mapana Kitaifa na hivyo wananchi kuvamia na kufanya shughuli zao katika eneo hilo inasababisha karantini hiyo kupoteza sifa yake kimataifa.
Pia, amekitaka Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala na Kampuni ya NARCO kuhakikisha inapima na kuweka alama kwenye mipaka ili kuepusha uvamizi katika maeneo yao.
Katibu Mkuu amelitaka Dawati la Ndege wafugwao kuanzisha Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ya Kuku na kuwapa vijana elimu juu ya Ufugaji bora wa kuku ili waweze kupata ajira, kujikwamua kiuchumi na kuongeza tija na Pato la Taifa kiujumla.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni