Na. Daudi Nyingo Dar Es Salaam.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb) amewataka watumishi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kutoa huduma zenye ubora, ufanisi pamoja na zinazotolewa kwa kasi inayotosheleza kwa kuzingatia heshima na uwajibikaji.
Dkt. Bashiru ameyasema hayo Desemba 06, 2025 alipotembelea Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyopo Temeke Dar Es Salaam akiongozana na Naibu Waziri Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (Mb) pamoja na Katibu Mkuu Bi. Agnes Meena kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali za kimaabara zinazofanywa na TVLA pamoja na kuongea na watumishi ili kutoa mwelekeo wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Muendelee kutoa huduma kwa umma kwa kuzingatia misingi ya haki, heshima, utu, uwajibikaji, kasi pamoja na uzalendo. Nimekuja kuwaahidi utendaji uliotukuka; niko hapa kuwaambia kwamba wizara na uongozi wake wapo tayari kushirikiana nanyi,” alisema Dkt. Bashiru.
“Tupo tayari kumuunga mkono Mhe. Rais ili atakapomaliza muhula wake wa uongozi aache tabasamu la utu kwa Watanzania kupitia wizara ya Mifugo na Uvuvi,” aliongeza.
Sambamba na hayo, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru aliwapongeza watumishi wa TVLA kwa kazi kubwa wanayoifanya kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na amewataka kudumisha mazuri yote yaliyopo kabla ya kuanzisha mapya, kwani amekuja kufanya mabadiliko mapya lakini kwa kuanzia na misingi mizuri aliyokuta. Alisema msingi wa maendeleo anayoyataka ili taifa liwe imara, lenye uchumi shirikishi na unaojitegemea, ni kuendeleza rasilimali watu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (Mb) alisema kuwa vijana wana jukumu la kujiendeleza kwani kwenye kundi kubwa kama la watumishi wa TVLA, ukiona watu wenye elimu ya juu lakini umri wao umekwenda kidogo, maana yake ni kuwa baada ya muda watatoka na vijana wanatakiwa kuchukua nafasi zao.
“Sifa kubwa ya vijana ni ubunifu. Tunategemea TVLA kuwa na watumishi wengi zaidi vijana ili kasi ya kazi na utoaji matokeo iwe kubwa zaidi, kwa njia fupi zaidi, kwa gharama ndogo lakini kwa matokeo makubwa. Tuzingatie uzalendo kwa nchi yetu; tuwe mabalozi wa kazi tunazozifanya, na tuchape kazi kwa moyo ili ifikapo 2030 tuwe tumewaweka wafugaji wote kwenye tabasamu,” alisema Mhe. Kamani.
Akitoa taarifa kwa Waziri, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 Wakala umeshuhudia mafanikio mengi yakiwemo ongezeko la mapato ya ndani kutoka bilioni 3.072 hadi bilioni 6.522, yaliyosababishwa na juhudi za menejimenti pamoja na watumishi katika kuhakikisha Wakala unasimama na kuwa chombo thabiti na kinachojitegemea.
Dkt. Bitanyi aliongeza kuwa Wakala imeongeza uzalishaji wa chanjo za mifugo kutoka dozi milioni 64.1 mwaka 2020/2021 hadi dozi milioni 82.6 kwa mwaka 2024/2025 ambayo ni hatua kubwa kwa TVLA. Sambamba na hilo, Wakala imeanzisha vituo viwili vya utoaji huduma za mifugo, ambavyo ni Kituo cha Meatu (Simiyu) na Kituo cha Sumbawanga (Rukwa). Aliongeza kuwa fanikio jingine ni kupata ithibati kwa vipimo 10 vya maabara, ambavyo hadi sasa TVLA inaendelea kuishikilia.


















































