Nav bar

Ijumaa, 28 Novemba 2025

DKT. BASHIRU AVUTIWA NA UWEKEZAJI SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

◼️Ahimiza Watumishi wa Wizara yake kuwajibika

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amevutiwa na uwekezaji uliofanywa na wadau wa sekta za Mifugo na Uvuvi nchini ambapo amewataka kushirikiana kwa ukaribu na Wizara yake ili kuendelea kuzalisha mazao yanayokidhi viwango stahiki.

Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa amesema hayo Novemba 27,2025 alipotembelea viwanda vya kusindika nyama (TANCHOICE na UNION MEAT) vyakula vya Mifugo na Samaki (BACKBONE)  na kiwanda cha kuzalisha chanjo (TANCHOICE) vilivyopo mkoani Pwani.

“Nipo tayari kuwapa ushirikiano wote mnaohitaji na mimi nimekuja kuomba ushirikiano wenu kwa sababu bila ushirikiano wetu kazi hii haiwezi kwenda inavyotakiwa na kila jambo mnaloona ni la mafanikio mtueleze ili tulidumishe na kila mnaliona ni dosari mtubainishie afu mtoe maoni ya namna ya kuondokana na vikwazo hivyo na kutatua dosari zilizopo kwa uzoefu mlionao” Ameongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Dkt. Bashiru ametoa wito kwa watumishi wa Wizara yake kuwajibika ipasavyo ili kuendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji hao kutimiza wajibu wao huku akisisitiza kutosita kuchukua hatua kwa mtendaji yoyote atakayezembea kwenye jambo hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani ameupongeza uongozi wa mkoa huo kwa kuweka mazingira wezeshi yaliyofanikisha uwepo wa Viwanda hivyo ambapo amefafanua kuwa jambo hilo linaakisi dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyolenga kufanya mageuzi ya uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji mkoani humo Bw. Ngobere Msamau ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajengea mazingira wezeshi ya kutekeleza shughuli zao kuwapatia ruzuku kwenye chanjo za Mifugo na kuwezesha uwekezaji wa viwanda cha kusindika nyama ambavyo  vimewafungulia soko la Mifugo yao. 

“Wajibu wetu kwa sasa ni kuendelea kuboresha mifugo yetu ili kuhakikisha viwanda hivi vinaendelea kupata malighafi za kutosha” Ameongeza Bw. Msamau.

Ziara ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu wake Mhe. Kamani itaendelea Novemba 28 mkoani Lindi ambapo wanatarajiwa kutembelea na kukagua hatua za ujenzi wa bandari ya Uvuvi iliyopo Wilaya ya Kilwa.

Meneja wa Shamba la uzalishaji malisho ya Mifugo la Vikuge Bw. Reuben Ngailo akimueleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) sifa za malisho ya Mifugo aina ya Nepia iliyoboreshwa (JUNCAO) muda mfupi baada ya Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa na Naibu  wake Mhe. Ng’wasi Kamani kufika (kushoto) kwenye shamba hilo lililopo mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani wakikagua kiwanda cha kusindika nyama cha Union Meat kilichopo eneo la Ruvu mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani wakioneshwa namna nyama inavyosindikwa kwenye kiwanda cha Union Meat kilichopo eneo la Ruvu mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akieleza umuhimu wa sekta za uzalishaji kwenye ukuzaji wa uchumi wa nchi wakati wa ziara yao na Mhe. Waziri Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa waliyoifanya mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akisalimiana na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon muda mfupi baada ya kuwasili mkoani humo Novemba 27,2025.




MRADI WA BBT WA UNENEPESHAJI MBUZI NA KONDOO KUANZA KUTEKELEZWA KONGWA

Na. Stanley Brayton, WMUV

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaanza Rasmi kutekeleza Mradi wa miaka Mitano wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ya Unenepeshaji wa Mbuzi na Kondoo katika eneo la Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) iliyopo Kongwa, ikiwa na lengo la kuongeza ushiriki wa Vijana na Wanawake katika ujasiliamali wa Biashara ya Mifugo.

Akizungumza wakati wa Ziara yake ya kikazi wakati akikagua Miundombinu ya Mradi huo, leo Novemba 27, 2025 Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amesema Mradi huo unatarajiwa kuanza kutoa Mafunzo mapema mwaka huu, na lengo la Mradi huo ni kwa ajili ya kuwapatia Vijana Mafunzo ya Unenepeshaji wa Mbuzi na Kondoo ili waweze kufuga kibiashara.

“mradi huu utakuwa na uwezo wa kutoa Mafunzo kwa vijana 200 kwa mwaka na vijana Takribani 1750 wataweza kupata Mafunzo hayo kwa miaka Mitano.” amesema Bi. Meena

Aidha, Bi. Meena amesema Mradi huo una eneo la heka 2000 kwa ajili ya kupanda Malisho ya Mifugo na hautokuwa wa unenepeshaji wa Mbuzi na Kondoo tu, bali utajumuisha kilimo cha Malisho ya Mifugo, uzalishaji wa nyama na vyakula vya Mifugo.

Vilevile, Bi. Meena amewataka Maafisa wa Wizara hiyo, kuboresha sehemu za michezo katika Mradi huo kama sehemu Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete na Mpira wa kikapu ili Vijana waweze kufanya mazoezi ili kujenga mwili baada ya shughuli za siku kuisha.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa kwanza kushoto), akiwa katika eneo la mabanda ya Mradi wa BBT ya Mbuzi na Kondoo wakati akifanya ukaguzi wa miundombinu hiyo, wakati wa Ziara  yake katika eneo la Mradi huo uliopo katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Uvuvi Tanzania (TALIRI) Kongwa, Novemba 27, 2025 Dodoma, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bwana. Daudi Mayeji.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa pili kushoto), akisikiliza hoja mbalimbali za Maafisa wa Wizara yake, juu ya uzalishaji wa tija na Uboreshaji wa Miundombinu mbalimbali, wakati alipotembelea na kufanya kikao kifupi na Maafisa hao katika Ofisi ya Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Uvuvi Tanzania (TALIRI) Kongwa, Novemba 27, 2025 Dodoma.


Mhandisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Mligo (aliyenyoosha Mkono), akielezea kwa mifano juu ya Ramani ya Majengo ya Mradi wa BBT uliopo katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Uvuvi Tanzania (TALIRI) Kongwa, wakati wa Ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Agnes Meena (hayupo pichani), Novemba 27, 2025 Dodoma.





DKT. BASHIRU AANZA KUWAPA ‘TABASAMU’ WAFUGAJI NCHINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Damas Kamani wameanza ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya Mifugo mkoani Morogoro ambapo wametembelea shamba la Mifugo na mfugaji Maloloi Kibangashi lililopo Wilayani Movemero.

Akizungumza mara baada ya kufika kwenye shamba la Bw. Maloloi Balozi Dkt. Bashiru mbali na kuvutiwa na kasi ya mabadiliko ya mfumo wa ufugaji aliyonayo mfugaji huyo kutoka kwenye ufugaji wa asili na kugeukia wa kisasa ambapo alitoa rai kwa wafugaji wengine kote nchini kuiga mfano huo.

“Wewe ni mmoja wa wafugaji wa kisasa ambao eneo lako limepangwa, limepimwa,limelindwa kisheria, lina maji, lina malisho na lina umeme na nimeambiwa ulianza kama mfugaji wa asili wa kawaida hivyo nimekuja kukuhakikishia wewe na wafugaji wote nchi nzima kwamba Wizara yangu itakuwa na ushirikiano na wafugaji wote na mimi pia nawaomba ushirikiano” Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Mhe. Dkt. Bashiru ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara yake inakusudia kuimarisha uzalishaji wa mifugo utakaozingatia upatikanaji wa uhakika wa malisho, maji, tiba na chanjo huku ikiendelea kuimarisha mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Ng’wasi Kamani amewataka wawekezaji wote kwenye sekta za Mifugo na Uvuvi kuhakikisha wanalinda fedha zote zilizotokana na kodi za Watanzania kwenye uwekezaji wao ili zitoe matokeo yaliyokusudiwa na Serikali.

“Pamoja na kwamba Mhe. Rais anaipenda sana Sekta binafsi na ametupa maelekezo mahsusi kwetu sisi wasaidizi wake kuwa lazima tuiangalie sekta hiyo kwa jicho jingine kwa sababu inaisaidia Serikali kufikisha huduma kwa wananchi wetu na kuingiza mapato hivyo ni lazima tuwe na ushirikiano wa karibu kati yetu, nyie wawekezaji na wananchi ili kuzipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zozote zinazojitokeza na kazi iendelee” Ameongeza Mhe. Kamani.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu wake Mhe. Kamani walihitimisha ziara yao kwa kutembelea kituo cha ukuzaji Viumbe Maji cha Kingolwira ambapo mbali na kuvutiwa na kinachoendelea kituoni hapo alitoa maelekezo ya kuhakikisha idara ya ukuzaji Viumbe Maji inafanya utafiti ili kuona uwezekano wa kupandikiza vifaranga vya samaki katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Ziara ya Viongozi hao itaendelea tena Novemba 27 katika mkoa wa Pwani ambapo itaanzia kwenye machinjio ya kisasa ya “Union Meat” iliyopo eneo la Ruvu.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani (kushoto) wakikagua shamba la Mifugo la mfugaji Maloloi Kibangashi Novemba 26,2025 Mvomero mkoani Morogoro.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akiwaeleza wafugaji dhamira ya Serikali kwenye uboreshaji wa sekta hiyo alipowatembelea Wilayani Mvomero (Morogoro) Novemba 26,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akihoji jambo mara baada ya kufika kwenye Machinjio ya kusindika Nyama ya  Nguru Hills iliyopo Manispaa ya Morogoro Novemba 26,2025. Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ng’wasi Kamani.








Jumamosi, 22 Novemba 2025

SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA WAVUVI KATIKA KUKUZA UCHUMI NCHINI - MHE. LIJUALIKALI

Na. Stanley Brayton, WMUV

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijualikali amesema Serikali inatambua mchango wa wavuvi katika kukuza uchumi nchini na ndio maana inaendelea kuboresha Miundombinu na maisha yao kwa kutoa mikopo ya boti za kisasa, vizimba na vitendea kazi vingine vitakavyowasaidia wavuvi kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ya uvuvi.

Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani, leo Novemba 21, 2025 katika Kijiji cha Kalungu kilichopo Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa, Mhe. Lijualikali amesema kuwa Maadhimisho hayo ni matokeo ya Dira na maono  thabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inachangia ipasavyo kwenye uchumi wa Taifa na kuinua kipato cha wananchi, hususan wavuvi wadogo na wakuzaji viumbe maji.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaendelea kuzipa kipaumbele Sekta za uzalishaji, ikiwemo Sekta ya Uvuvi." alisema Mhe. Lijualikali

Aidha, Mhe. Lijualikali amebainisha kuwa Sekta ya Uvuvi ni miongoni mwa nguzo muhimu ya kukuza uchumi nchini kwani inachangia ajira, uhakika wa upatikanaji wa lishe Bora na chakula, kipato kwa familia na Taifa

Vilevile, Mhe. Lijualikali ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (TNC), kwa kuwezesha Maadhimisho hayo kufanyika.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Dkt. Baraka Sekadende amesema kuwa lengo la Maadhimisho hayo ni kuwaleta wadau wa Uvuvi pamoja, kusikiliza hoja, kero, mawazo yao, kubadilishana mawazo na uzoefu baina ya wadau wa Sekta na Wizara, pamoja na kuelimisha Wavuvi kuhusu mabadiriko ya Sheria, Kanuni, Miongozo na Mipango iliyopo.

Pia, Dkt. Baraka Sekadende amewataka wavuvi wote kuungana kwa pamoja kusherekea siku hii ili kufikia muafaka wa namna ya kufanya shughuli za uvuvi kwa njia endelevu na tija.

Naye, Mwakilishi wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (TNC), Bw. John Kimaro amesema ni vyema wavuvi kuhakikisha Mazingira ya fukwe za Ziwa Tanganyika zinakuwa safi ili kuzuia uchafuzi kwani kuna athari kubwa ziwa likichafuka ikiwemo viumbe vya majini kupoteza uhai, ubora wake na kuathiri afya ya mlaji.

Bw. Kimaro amesema ni vyema wavuvi kujenga tabia ya kufanya usafi mara kwa mara katika fukwe hizo ili kuhakikisha Ziwa Tanganyika linakuwa salama kwa sasa hadi kizazi cha baadae.

Diwani Mteule wa Mkinga Wilayani Nkasi, Mhe. Mohamed Zaidi ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwajali wavuvi kwa kuwajengea miundombinu bora ambayo imekuwa msaada tosha katika shughuli zao za uzalishaji na kusaidia kuimarisha uchumi wa wavuvi na nchi kiujumla.

Mhe. Zaidi amebainisha kuwa kwa sasa wavuvi wa Mkinga wana uhitaji wa Soko la kuuzia Samaki, boti za kisasa, Vizimba vya kufugia Samaki pamoja na zana zingine za uvuvi ili kuongeza uzalishaji zaidi wa zao hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijualikali, akihutubia wadau wa Sekta ya Uvuvi, katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani, iliyofanyika katika Kijiji cha Kalungu, Novemba 21, 2025, Nkasi - Rukwa.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Dkt. Baraka Sekadende (wa pili kushoto) na Diwani Mteule wa Kata ya Mkinga Wilayani Nkasi, Mhe. Mohamed Zaidi (wa tatu kushoto) wakitoa zawadi ya fedha taslim kiasi cha Shilingi laki Moja na Ishirini kwa kikundi cha Wanaume Wavuvi kilichoibuka Mshindi wa kwanza wa mbio za kasi katika kuendesha Mtumbwi, katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani, iliyofanyika katika Kijiji cha Kalungu, Novemba 21, 2025, Nkasi - Rukwa.

Diwani Mteule wa Kata ya Mkinga Wilayani Nkasi, Mhe. Mohamed Zaidi (katikati) akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Dkt. Baraka Sekadende (wa kwanza kushoto), Risala ya Wavuvi wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Mkinga (FICOS), katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani, iliyofanyika katika Kijiji cha Kalungu, Novemba 21, 2025, Nkasi - Rukwa.

Picha ni Kikundi cha Wanawake Wavuvi wakiwa kwenye mashindano ya mbio za kasi katika kuendesha Mtumbwi, katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani, iliyofanyika katika Kijiji cha Kalungu, Novemba 21, 2025, Nkasi - Rukwa.

Picha ni baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi wakimsikiliza Mgeni Rasmi (hayupo pichani), katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani, iliyofanyika katika Kijiji cha Kalungu, Novemba 21, 2025, Nkasi - Rukwa.




MAUZO YA SAMAKI YAPAA NJE YA NCHI

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, Novemba 21, 2025, alipokuwa akihitimisha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach kwa lengo la kuhamasisha dhana ya Uchumi wa Buluu, ulaji wa samaki na mazao yake, pamoja na kuimarisha shughuli za uhifadhi wa mazingira na rasilimali za uvuvi yaliyofanyika kwa muda wa siku 2 kuanzia tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025.

Akizungumza wakati wa hotuba yake, Bi. Meena alisema kuwa uuzaji wa samaki nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 42,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 509.9 hadi tani 59,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 755. Sambamba na hilo, idadi ya wavuvi imeongezeka kutoka 198,475 mwaka 2023 hadi 201,661 mwaka 2024. Idadi ya viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi nayo imeongezeka kutoka 21 hadi 64 katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024.

“Sisi sote tunafahamu kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za maji ikiwemo bahari, mito, mabwawa, maziwa na maeneo oevu, ambazo ni nguzo muhimu za uchumi wa buluu. Watanzania wapatao milioni sita wanategemea shughuli za uvuvi katika kujipatia kipato. Tukizingatia kuwa nchi ina jumla ya takribani watu milioni 62 hadi 63, ina maana kuwa asilimia 10 ya Watanzania wanategemea sekta hii—jambo linaloonyesha umuhimu wake kwa uchumi wa taifa.”

“Serikali itaendelea kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, ufugaji wa samaki kwa njia za vizimba na mabwawa, pamoja na kuandaa na kutekeleza mikakati na mipango ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi ili kuongeza uzalishaji wa samaki, kupunguza uharibifu wa mazingira, kuzuia uvamizi wa fukwe na kupunguza shinikizo la uvuvi,” alisema Bi. Meena.

Sambamba na hayo, Katibu Mkuu alisema kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi ili kuimarisha usalama wa chakula, lishe, kipato cha kaya na uchumi wa taifa. Kutokana na juhudi hizo, tumeshuhudia ongezeko la uzalishaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 479,976 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 mwaka 2023 hadi tani 522,788 zenye thamani ya shilingi trilioni 4.3 mwaka 2024.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Emelda Teikwa, amesema kuwa wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamefanya maadhimisho haya katika mkoa wa Dar es Salaam na Rukwa. Ameongeza kuwa Siku ya Mvuvi Duniani imekuwa ikitumika kama jukwaa la kujenga uelewa kwa wavuvi na kuelimisha kuhusu uhifadhi wa mazingira na usafi wa fukwe, na pia kuelimisha kuhusu uvuvi endelevu.

Bi. Teikwa aliongeza kuwa katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu, wizara imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya jamii.

Akitoa salamu kwa niaba ya wavuvi, Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) eneo la Kawe Beach, Bw. Mudu Mohamed, ameiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti uvamizi wa fukwe ambao umeanza kukithiri katika maeneo ya Kawe, Kunduchi, Msasani, Mbweni na Ununio.

Bw. Mudu amesema uvamizi huo unaathiri shughuli za uvuvi na kuhatarisha ustahimilivu wa mazingira sambamba na kuhatarisha fursa za kibiashara kwa akina mama na vijana wanaotegemea fukwe hizo. Ameomba Serikali kuhakikisha suala hilo linasimamiwa kwa umakini na haraka, sambamba na kuwaongezea BMU boti moja ya uvuvi itakayosaidia kufanikisha doria, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za bahari na kulinda mazingira ya fukwe.

Katika siku ya kwanza ya maadhimisho (20 Novemba 2025), shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo kampeni za uhifadhi wa mazingira, kufanya usafi wa fukwe, midahalo iliyowawezesha wavuvi kupata elimu na kuuliza maswali mbalimbali, pamoja na uhamasishaji wa ulaji wa samaki kwa manufaa ya afya na uchumi.

Sambamba na hayo, Katibu Mkuu amezindua mpango wa kitaifa wa usimamizi wa samaki aina ya Jodari na mpango wa uhifadhi wa samaki aina ya papa na taa, pamoja na kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho kujionea bidhaa za mazao ya uvuvi.

Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu isemayo “Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Endelevu: Msingi Imara wa Uchumi wa Buluu.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, akiongea na wadau wa Uvuvi na Mazingira Novemba 21, 2025 alipokuwa akihitimisha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (katikati) akizindua mpango wa kitaifa wa usimamizi wa samaki aina ya Jodari na mpango wa uhifadhi wa samaki aina ya papa na taa Novemba 21, 2025 alipokuwa akihitimisha kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena akitembelea baadhi ya mabanda ya maonesho ya bidhaa mbalimbali za mazao ya Uvuvi yanayotengenezwa na wajasiliamali Novemba 21, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.

Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) eneo la Kawe Beach, Bw. Mudu Mohamed akisoma risala kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena Novemba 21, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.

Wadau mbalimbali wa Uvuvi na Mazingira wakisikiliza hutuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena (hayupo pichani) Novemba 21, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.




DKT. BASHIRU AANIKA MWELEKEO WA SEKTA YA MIFUGO KWA WAFUGAJI

◼️Ni katika mkutano wake na Chama cha Wafugaji nchini

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amekutana na Sekretarieti ya Chama cha wafugaji nchini ikiwa ni takribani siku mbili tu tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo ambapo amewaelekeza kuhakikisha wanalinda mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta ya Mifugo.

Katika kikao hicho kilichofanyika Novemba 20,2025 kwenye Ofisi za Wizara hiyo zilizopo eneo la Mtumba jijini Dodoma, Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa sekta za uzalishaji ikiwemo Mifugo na Uvuvi ndio nguzo ya kulifanya Taifa lijitegemee kiuchumi na kutekeleza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Dkt. Sami Suluhu Hassan.

“Tunategemea sekta ya Ufugaji itoe mchango mkubwa katika uendeshaji na ukuzaji wa uchumi wetu na kuboresha maisha ya watu wetu” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru ameelekeza kutoanzishwa kwa miradi mipya Wizarani hapo hadi itakapokamilishwa ile iliyoanzishwa awali na kuanza kufanya kazi iliyokusudiwa.

“Najua ipo miradi imekamilika lakini haijaanza kufanya kazi hivyo tutafanya uchambuzi tuainishe maeneo ambayo tayari fedha za umma zimeshawekezwa na malengo yalikuwepo lakini miradi hiyo haijaanza kuleta matokeo ili tuhakikishe inafanya kazi na ile ambayo haijakamilika tunakamilisha na wakati huo huo tunaanza miradi mipya na hayo ni maelekezo ya Mhe. Rais kwa sekta zote ” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini Bw. Murida Mshota amemuahidi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu Wake Mhe. Ng’wasi Kamani kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote watakachohudumu katika nafasi hiyo ambapo pia aliwakabidhi viongozi hao rasimu ya wafugaji inayoelezea mipango mbalimbali ya uboreshaji wa sekta hiyo inayotarajiwa kutekelezwa na wafugaji kote nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani wakionesha rasimu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta ya Mifugo iliyoandaliwa na inayotarajiwa kutekelezwa na Chama cha Wafugaji nchini wakati wa kikao chao na Sekretarieti ya Chama hicho Novemba 20,2025 Mtumba jijini Dodoma.



Alhamisi, 20 Novemba 2025

MRADI WA UZALISHAJI MBEGU BORA ZA NG’OMBE WA MAZIWA MBIONI KUTEKELEZWA NCHINI

◼️Utagharimu takribani Shilingi Bil. 7

◼️ Umefadhiliwa na Shirika la kimataifa la Ushirikiano wa Maendeleo la Korea (KOICA)

Nchi ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine na timu ya Watafiti kutoka chuo kikuu cha Jeonbuk nchini Korea inatarajia kutekeleza mradi wa utafiti na uzalishaji wa ng’ombe wa Maziwa kwa kutumia teknolojia za Uhimilishaji na Uhawilishaji wa viini tete.

Hayo yamebainishwa na Ujumbe wa Wawakilishi kutoka chuo kikuu cha Jeonbuk nchini Korea Prof.  Hakkyo Lee, Mwondha Faluku na Rais wa Taasisi ya CACOON Bw. HeeJae ulioongozwa na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya ambao walifika ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Agness Meena kwa ajili ya kutambulisha azma ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe huo, Bi. Meena amewataka wataalam hao kukaa pamoja na wataalam wa Wizara yake na kuwashirikisha wadau wengine wanaohusika na utekelezaji wa miradi nchini ili kujadili hatua sahihi za kufuata kabla ya utekelezaji wa mradi huo.

“Kwa kuwa ndo mpo kwenye hatua ya usanifu wa mradi ni vema wataalam wetu wakashiriki kikamilifu ili kuona ni maeneo gani tunahitaji kunifaika zaidi kupitia mradi huo” Amesema Bi. Meena.

Kwa upande Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya ameeleza kuwa mradi huo utasaidia wafugaji nchini kupata mbegu bora za Ng’ombe wa maziwa hatua ambayo itaongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa nchini na kuhamasisha ufugaji unaotunza mazingira.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena akisalimiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Jeonbuk (JBNU) cha Korea muda mfupi baada ya kufika ofisini kwake eneo la Mtumba jijini Dodoma Novemba 19,2025.

Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya (mbele) akieleza namna mradi wa uzalishaji wa ng’ombe wa kisasa wa Maziwa utakavyowanufaisha wafugaji nchini muda mfupi baada ya kufika ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena Novemba 19,2025 Mtumba, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Jeonbuk (JBNU) cha Korea na Wataalam wa Wizara yake muda mfupi baada ya kukamilika kwa mazungumzo baina yao Novemba 19,2025 Mtumba, jijini Dodoma.


TUTATEKELEZA MAONO YA MHESHIMIWA RAIS DKT. SAMIA - BALOZI DKT. BASHIRU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa juhudi ili kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya sekta hizo za uzalishaji.

Dkt. Kakurwa amesema hayo mara baada ya kupokelewa na Watumishi wa Wizara hiyo Novemba 18,2025  Wizarani hapo ikiwa ni muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo.

"Sote tumesikia aliyosema Mhe. Rais kupitia hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge kuhusu sekta zetu za Mifugo na Uvuvi hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunatekekeza maono hayo kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kwa nafasi aliyonayo" Amesema Dkt. Bashiru.

Aidha Dkt. Bashiru amewataka watumishi hao kutoa ushirikiano wa kutosha kwake na Naibu Waziri Mhe. Ng'wasi Kamani katika kipindi chote cha kuwahudumia wananchi hususan wadau wa sekta za Mifugo na Uvuvi. 

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu wake Mhe. Kamani waliteuliwa na Rais Samia kushika nyadhifa hizo Novemba 17,2025.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena akimkabidhi Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa nyaraka za utendaji wa ofisi yake Makao makuu ya Wizara hiyo Novemba 18,2025 Mtumba jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena akimkabidhi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani nyaraka za utendaji wa ofisi yake Makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma Novemba 18,2025.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena akimuongoza ofisini kwake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani muda mfupi baada ya kuwasili makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma Novemba 18,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akisaini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kuwasili na kupokelewa Makao Makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma Novemba 18,2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani akisaini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kuwasili na kupokelewa Makao Makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma Novemba 18,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akila kiapo cha kutumikia nafasi hiyo Novemba 18,2025 Ikulu jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani akila kiapo cha kutumikia nafasi hiyo Novemba 18,2025 Ikulu jijini Dodoma.




SERIKALI YA AWAMU YA SITA, YADHAMIRIA KUIMARISHA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Na. Stanley Brayton - Dodoma

◾ Yaongeza eneo la ufugaji kutoka ekari milioni 3.46 hadi Milioni 6.

◾ Yaahidi kuendeleza chanjo za mifugo, kuboresha kosafu ya mifugo, ujenzi wa majosho na machinjio.

◾ Kujenga bandari ya uvuvi ya Bagamoyo na kukamilisha bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo itatoa fursa za ajira takriban 30,000.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga vyema kuimarisha sekta za mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na kutoa fursa kwa Vijana na wadau wote ili kukuza kipato chao na kipato cha Taifa kiujumla.

Akizungumza wakati wa kuhutubia na kufungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mkutano wa kwanza kikao cha nne cha Bunge hilo, jijini Dodoma )14.11.2025), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mikakati ya kukuza sekta ya mifugo katika muhula wa pili wa serikali ya awamu ya sita ni pamoja na kuongeza eneo lililopimwa la shughuli za ufugaji kutoka ekari milioni 3.46 hadi ekari milioni 6 ili kuepusha migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, pamoja na kuongeza wigo wa uzalishaji wa malisho ya mifugo ili kuelekea kwenye ufugaji wa kisasa. 

"katika hatua ya kufungua masoko ya kimataifa, serikali itaendeleza chanjo pamoja na utambuzi wa mifugo nchini ili kuongeza ubora wa mazao ya mifugo na kuingia katika kumbukumbu za dunia na kutambulika sokoni." amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan 

Aidha, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kuboresha kosaafu ya mifugo, kujenga mabwawa ya kunyweshea mifugo, majosho, machinjio na miundombinu mingine muhimu kwa ajili ya ufugaji, ikiwa na lengo la kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo na kufungua masoko ya nje ili wafugaji watoke kumtazama ng'ombe na mlio wake bali kwa kutazama uzito wa nyama, ladha, wingi wa maziwa, ubora wa ngozi, kwato na pembe za ng'ombe, ambayo ndiyo itakayoleta mapinduzi ya sekta ya mifugo.

Vilevile, Mhe. Dkt. Samia  amebainisha kuwa katika sekta ya uvuvi serikali itaendelea kuelekaza manufaa ya uvuvi wa bahari kuu na kwenye maziwa makuu kwa kukamilisha mradi wa bandari kuu ya uvuvi ya Kilwa Masoko iliyopo mkoani Lindi ambayo itazalisha fursa ya ajira takriban 30,000 na kujenga bandari nyingine Bagamoyo mkoani Pwani, ambayo itafunganishwa na kongani ya viwanda vya samaki.

Pia, ameweka wazi kuwa serikali ya awamu ya sita itafanya mapitio ya leseni za uvuvi kwa lengo la kuifanya nchi na wavuvi waweze kufaidika ipasavyo na fursa za uvuvi wa bahari kuu, pamoja na kutoa mikopo ya boti, dhana za uvuvi, makasha ya kuifadhi samaki na miundombinu ya kukaushia bidhaa hizo.

Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukuza sekta ya uvuvi kwa kuwekeza zaidi kwenye ufugaji kwa njia ya vizimba na mabwawa ya kufugia samaki ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa kufungua Rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkutano wa kwanza Kikao cha Nne, kilichofanyika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba 14, 2025 Dodoma.