Nav bar

Ijumaa, 28 Novemba 2025

MRADI WA BBT WA UNENEPESHAJI MBUZI NA KONDOO KUANZA KUTEKELEZWA KONGWA

Na. Stanley Brayton, WMUV

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaanza Rasmi kutekeleza Mradi wa miaka Mitano wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ya Unenepeshaji wa Mbuzi na Kondoo katika eneo la Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) iliyopo Kongwa, ikiwa na lengo la kuongeza ushiriki wa Vijana na Wanawake katika ujasiliamali wa Biashara ya Mifugo.

Akizungumza wakati wa Ziara yake ya kikazi wakati akikagua Miundombinu ya Mradi huo, leo Novemba 27, 2025 Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amesema Mradi huo unatarajiwa kuanza kutoa Mafunzo mapema mwaka huu, na lengo la Mradi huo ni kwa ajili ya kuwapatia Vijana Mafunzo ya Unenepeshaji wa Mbuzi na Kondoo ili waweze kufuga kibiashara.

“mradi huu utakuwa na uwezo wa kutoa Mafunzo kwa vijana 200 kwa mwaka na vijana Takribani 1750 wataweza kupata Mafunzo hayo kwa miaka Mitano.” amesema Bi. Meena

Aidha, Bi. Meena amesema Mradi huo una eneo la heka 2000 kwa ajili ya kupanda Malisho ya Mifugo na hautokuwa wa unenepeshaji wa Mbuzi na Kondoo tu, bali utajumuisha kilimo cha Malisho ya Mifugo, uzalishaji wa nyama na vyakula vya Mifugo.

Vilevile, Bi. Meena amewataka Maafisa wa Wizara hiyo, kuboresha sehemu za michezo katika Mradi huo kama sehemu Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete na Mpira wa kikapu ili Vijana waweze kufanya mazoezi ili kujenga mwili baada ya shughuli za siku kuisha.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa kwanza kushoto), akiwa katika eneo la mabanda ya Mradi wa BBT ya Mbuzi na Kondoo wakati akifanya ukaguzi wa miundombinu hiyo, wakati wa Ziara  yake katika eneo la Mradi huo uliopo katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Uvuvi Tanzania (TALIRI) Kongwa, Novemba 27, 2025 Dodoma, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bwana. Daudi Mayeji.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa pili kushoto), akisikiliza hoja mbalimbali za Maafisa wa Wizara yake, juu ya uzalishaji wa tija na Uboreshaji wa Miundombinu mbalimbali, wakati alipotembelea na kufanya kikao kifupi na Maafisa hao katika Ofisi ya Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Uvuvi Tanzania (TALIRI) Kongwa, Novemba 27, 2025 Dodoma.


Mhandisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Mligo (aliyenyoosha Mkono), akielezea kwa mifano juu ya Ramani ya Majengo ya Mradi wa BBT uliopo katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Uvuvi Tanzania (TALIRI) Kongwa, wakati wa Ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Agnes Meena (hayupo pichani), Novemba 27, 2025 Dodoma.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni