Nav bar

Ijumaa, 28 Novemba 2025

DKT. BASHIRU AVUTIWA NA UWEKEZAJI SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

◼️Ahimiza Watumishi wa Wizara yake kuwajibika

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amevutiwa na uwekezaji uliofanywa na wadau wa sekta za Mifugo na Uvuvi nchini ambapo amewataka kushirikiana kwa ukaribu na Wizara yake ili kuendelea kuzalisha mazao yanayokidhi viwango stahiki.

Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa amesema hayo Novemba 27,2025 alipotembelea viwanda vya kusindika nyama (TANCHOICE na UNION MEAT) vyakula vya Mifugo na Samaki (BACKBONE)  na kiwanda cha kuzalisha chanjo (TANCHOICE) vilivyopo mkoani Pwani.

“Nipo tayari kuwapa ushirikiano wote mnaohitaji na mimi nimekuja kuomba ushirikiano wenu kwa sababu bila ushirikiano wetu kazi hii haiwezi kwenda inavyotakiwa na kila jambo mnaloona ni la mafanikio mtueleze ili tulidumishe na kila mnaliona ni dosari mtubainishie afu mtoe maoni ya namna ya kuondokana na vikwazo hivyo na kutatua dosari zilizopo kwa uzoefu mlionao” Ameongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Dkt. Bashiru ametoa wito kwa watumishi wa Wizara yake kuwajibika ipasavyo ili kuendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji hao kutimiza wajibu wao huku akisisitiza kutosita kuchukua hatua kwa mtendaji yoyote atakayezembea kwenye jambo hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani ameupongeza uongozi wa mkoa huo kwa kuweka mazingira wezeshi yaliyofanikisha uwepo wa Viwanda hivyo ambapo amefafanua kuwa jambo hilo linaakisi dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyolenga kufanya mageuzi ya uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji mkoani humo Bw. Ngobere Msamau ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajengea mazingira wezeshi ya kutekeleza shughuli zao kuwapatia ruzuku kwenye chanjo za Mifugo na kuwezesha uwekezaji wa viwanda cha kusindika nyama ambavyo  vimewafungulia soko la Mifugo yao. 

“Wajibu wetu kwa sasa ni kuendelea kuboresha mifugo yetu ili kuhakikisha viwanda hivi vinaendelea kupata malighafi za kutosha” Ameongeza Bw. Msamau.

Ziara ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu wake Mhe. Kamani itaendelea Novemba 28 mkoani Lindi ambapo wanatarajiwa kutembelea na kukagua hatua za ujenzi wa bandari ya Uvuvi iliyopo Wilaya ya Kilwa.

Meneja wa Shamba la uzalishaji malisho ya Mifugo la Vikuge Bw. Reuben Ngailo akimueleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) sifa za malisho ya Mifugo aina ya Nepia iliyoboreshwa (JUNCAO) muda mfupi baada ya Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa na Naibu  wake Mhe. Ng’wasi Kamani kufika (kushoto) kwenye shamba hilo lililopo mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani wakikagua kiwanda cha kusindika nyama cha Union Meat kilichopo eneo la Ruvu mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani wakioneshwa namna nyama inavyosindikwa kwenye kiwanda cha Union Meat kilichopo eneo la Ruvu mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akieleza umuhimu wa sekta za uzalishaji kwenye ukuzaji wa uchumi wa nchi wakati wa ziara yao na Mhe. Waziri Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa waliyoifanya mkoani Pwani Novemba 27,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akisalimiana na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon muda mfupi baada ya kuwasili mkoani humo Novemba 27,2025.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni