Nav bar

Alhamisi, 20 Novemba 2025

MRADI WA UZALISHAJI MBEGU BORA ZA NG’OMBE WA MAZIWA MBIONI KUTEKELEZWA NCHINI

◼️Utagharimu takribani Shilingi Bil. 7

◼️ Umefadhiliwa na Shirika la kimataifa la Ushirikiano wa Maendeleo la Korea (KOICA)

Nchi ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine na timu ya Watafiti kutoka chuo kikuu cha Jeonbuk nchini Korea inatarajia kutekeleza mradi wa utafiti na uzalishaji wa ng’ombe wa Maziwa kwa kutumia teknolojia za Uhimilishaji na Uhawilishaji wa viini tete.

Hayo yamebainishwa na Ujumbe wa Wawakilishi kutoka chuo kikuu cha Jeonbuk nchini Korea Prof.  Hakkyo Lee, Mwondha Faluku na Rais wa Taasisi ya CACOON Bw. HeeJae ulioongozwa na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya ambao walifika ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Agness Meena kwa ajili ya kutambulisha azma ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe huo, Bi. Meena amewataka wataalam hao kukaa pamoja na wataalam wa Wizara yake na kuwashirikisha wadau wengine wanaohusika na utekelezaji wa miradi nchini ili kujadili hatua sahihi za kufuata kabla ya utekelezaji wa mradi huo.

“Kwa kuwa ndo mpo kwenye hatua ya usanifu wa mradi ni vema wataalam wetu wakashiriki kikamilifu ili kuona ni maeneo gani tunahitaji kunifaika zaidi kupitia mradi huo” Amesema Bi. Meena.

Kwa upande Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya ameeleza kuwa mradi huo utasaidia wafugaji nchini kupata mbegu bora za Ng’ombe wa maziwa hatua ambayo itaongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa nchini na kuhamasisha ufugaji unaotunza mazingira.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena akisalimiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Jeonbuk (JBNU) cha Korea muda mfupi baada ya kufika ofisini kwake eneo la Mtumba jijini Dodoma Novemba 19,2025.

Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya (mbele) akieleza namna mradi wa uzalishaji wa ng’ombe wa kisasa wa Maziwa utakavyowanufaisha wafugaji nchini muda mfupi baada ya kufika ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena Novemba 19,2025 Mtumba, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Jeonbuk (JBNU) cha Korea na Wataalam wa Wizara yake muda mfupi baada ya kukamilika kwa mazungumzo baina yao Novemba 19,2025 Mtumba, jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni