Na. Stanley Brayton, WMUV
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijualikali amesema Serikali inatambua mchango wa wavuvi katika kukuza uchumi nchini na ndio maana inaendelea kuboresha Miundombinu na maisha yao kwa kutoa mikopo ya boti za kisasa, vizimba na vitendea kazi vingine vitakavyowasaidia wavuvi kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ya uvuvi.
Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani, leo Novemba 21, 2025 katika Kijiji cha Kalungu kilichopo Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa, Mhe. Lijualikali amesema kuwa Maadhimisho hayo ni matokeo ya Dira na maono thabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inachangia ipasavyo kwenye uchumi wa Taifa na kuinua kipato cha wananchi, hususan wavuvi wadogo na wakuzaji viumbe maji.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaendelea kuzipa kipaumbele Sekta za uzalishaji, ikiwemo Sekta ya Uvuvi." alisema Mhe. Lijualikali
Aidha, Mhe. Lijualikali amebainisha kuwa Sekta ya Uvuvi ni miongoni mwa nguzo muhimu ya kukuza uchumi nchini kwani inachangia ajira, uhakika wa upatikanaji wa lishe Bora na chakula, kipato kwa familia na Taifa
Vilevile, Mhe. Lijualikali ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (TNC), kwa kuwezesha Maadhimisho hayo kufanyika.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Dkt. Baraka Sekadende amesema kuwa lengo la Maadhimisho hayo ni kuwaleta wadau wa Uvuvi pamoja, kusikiliza hoja, kero, mawazo yao, kubadilishana mawazo na uzoefu baina ya wadau wa Sekta na Wizara, pamoja na kuelimisha Wavuvi kuhusu mabadiriko ya Sheria, Kanuni, Miongozo na Mipango iliyopo.
Pia, Dkt. Baraka Sekadende amewataka wavuvi wote kuungana kwa pamoja kusherekea siku hii ili kufikia muafaka wa namna ya kufanya shughuli za uvuvi kwa njia endelevu na tija.
Naye, Mwakilishi wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (TNC), Bw. John Kimaro amesema ni vyema wavuvi kuhakikisha Mazingira ya fukwe za Ziwa Tanganyika zinakuwa safi ili kuzuia uchafuzi kwani kuna athari kubwa ziwa likichafuka ikiwemo viumbe vya majini kupoteza uhai, ubora wake na kuathiri afya ya mlaji.
Bw. Kimaro amesema ni vyema wavuvi kujenga tabia ya kufanya usafi mara kwa mara katika fukwe hizo ili kuhakikisha Ziwa Tanganyika linakuwa salama kwa sasa hadi kizazi cha baadae.
Diwani Mteule wa Mkinga Wilayani Nkasi, Mhe. Mohamed Zaidi ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwajali wavuvi kwa kuwajengea miundombinu bora ambayo imekuwa msaada tosha katika shughuli zao za uzalishaji na kusaidia kuimarisha uchumi wa wavuvi na nchi kiujumla.
Mhe. Zaidi amebainisha kuwa kwa sasa wavuvi wa Mkinga wana uhitaji wa Soko la kuuzia Samaki, boti za kisasa, Vizimba vya kufugia Samaki pamoja na zana zingine za uvuvi ili kuongeza uzalishaji zaidi wa zao hilo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni