Nav bar

Ijumaa, 2 Januari 2026

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU NYAVU HARAMU ZA DAGAA

◼️Taa za umeme wa jua zawekwa kiporo

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepiga marufuku matumizi ya nyavu za uvuvi zilizolalamikiwa na Wavuvi kuwa zinachangia kuongezeka kwa Uvuvi haramu.

Marufuku hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa wakati wa mkutano wake na wadau mbalimbali wa Uvuvi uliofanyika jijini Mwanza Desemba 24,2025.

“Kwa hiyo ninaelekezea haya mawili moja la Taa naomba zifanyiwe utafiti ndani ya wiki 2 kwa sababu tafiti zipo ni kuzichambua tu kisha ntalitoea maelekezo lakini hili la nyavu haramu za dagaa halina masihara wala msalimie mtume,tutafute nyavu ambazo zinaweza kuturuhusu tuvue uvuvi endelevu na tubaki kazini na nchi yetu ibaki salama” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa kufuatia marufuku hiyo Serikali itaweka vyombo vyake kwenye mipaka yote ili kuzuia nyavu hizo zisiingie nchini.

Awali wakizungumza wakati wa Mkutano huo, baadhi ya Wavuvi walimueleza Balozi Dkt. Bashiru kuwa nyavu hizo za dagaa zimekuwa zikivua mpaka mazalia ya samaki aina ya sangara kwa kiwango kikubwa huku pia wakimlalamikia matumizi ya taa zinazotumia umeme wa jua kuwa mwanga wake ni mkali na unavuta hata samaki wasiotakiwa kuvuliwa.

Kabla ya kuelekea kwenye mkutano huo Balozi Dkt. Bashiru alishiriki kupandikiza samaki katika eneo la Shadi lililopo Wilaya ya Nyamagana mkoani humo ambapo aliwaeleza wakazi wa eneo hilo kuwa Serikali itapeleka vizimba vya kufugia samaki katika eneo hilo ili kuendelea kulinda samaki wa asili waliopo hapo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akipandikiza vifaranga vya samaki ndani ya Ziwa Victoria kwenye eneo la Shadi lililopo Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Desemba 24,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akizungumza na Mkurugenzi wa Uvuvi nchini Prof. Mohammed Sheikh (kushoto) wakati wakikagua shughuli za Uvuvi wa ziwa Victoria mkoani Mwanza Desemba 24,2025. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda mara baada ya kufika ofisini kwake Desemba 24,2025.

Pichani ni Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa wadau wa Uvuvi uliofanyika Desemba 24,2025 jijini Mwanza ambapo Serikali ilitangaza kupiga marufuku nyavu za kuvulia samaki maarufu kama “nyavu za kijapan”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni