Na, Hamisi Hussein, Singida
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambae pia ni Mbunge wa Kundi la Vijana kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Ng'wasi Damas Kamani, amesema ataendelea kulisemea, kulitetea na kulipambania kundi la vijana kupata fursa mbalimbali za kujiinua kiuchumi hususani katika sekta ya mifugo na uvuvi.
Mhe. Ng'wasi ameyasema hayo leo Desemba, 24, 2025, Wilayani Iramba Mkoani Singida, alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika Kikao cha Baraza la Kawaida la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo.
"Pamoja na majukumu haya niliyopewa sitachoka kumtetea, kumsemea na kumpambania kijana wa kitanzania, lakini pia hata katika sekta hii ninayoisimamia huku ndio nitaweka nguvu zaidi ili ikiwezekana na sekta zingine ziige kutoka kwetu namna ya kumsaidia kijana wa kitanzania"amesema N'gwasi.
Katika hatua nyingine Mhe. Ng'wasi amesema yuko tayari kushirikiana na vijana katika kuzifikia fursa za kiuchumi na kuwahimiza vijana hususani wa Chama cha Mapinduzi kuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani nchini pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Mhe. Rais Samia ametuamini vijana na ametupa nafasi ili masuala yanayohusu vijana tuyaamue wenyewe, ni jukumu letu kumuombea Rais wetu na taifa letu kwa ujumla,kukemea hadharani vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi watu" aliongeza Mhe. Ng'wasi.
Awali akisoma taarifa ya Chama Katibu wa UVCCM Wilaya ya Iramba Bw. Amani Daudi amesema zaidi ya vikundi 31 vimenufika na fedha za asilimia 10 za halmashauri ambapo jumuiya ya umoja wa vijana imepata shilingi miloni 207.7.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni