Serikali ya kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mifugo imeanza kufanya mapitio ya kutokomeza ugonjwa Sotoka (Peste des Petits Ruminants (PPR) ifikapo mwaka 2030, hatua itakayoiweka Tanzania katika mstari wa mbele barani Afrika katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu unaodhuru mifugo.
Akifungua warsha ya Kitaifa ya Tathmini na Mapitio ya Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na PPR iliyofanyika leo Desemba Mosi, 2025 katika Hoteli ya Peacok jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi.Agnes Meena amesema Sekta ya mifugo imekuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, ikichangia asilimia 6.2 ya Pato la Taifa na kusaidia zaidi ya kaya milioni tano lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa yanayosababisha vifo vya mifugo.
“Kondoo na mbuzi wanakabiliwa na changamoto ya PPR inayosababisha vifo vingi, hasara za kiuchumi na kukwamisha upatikanaji wa masoko ya kikanda na kimataifa.”
Bi. Meena aliongeza kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa miaka mitano ijayo ili kuimarisha chanjo, utambuzi na mifumo ya ufuatiliaji wa mifugo, hivyo dhamira ya serikali kutokomeza magonjwa ya mifugo ikiwemo PPR itafanikiwa.
Hapo awali, Mwakilishi wa Shirika la Rasilimali za Mifugo la Umoja wa Africa (AU-IBAR) Dkt. Folorunso Fasina, alibainisha nafasi muhimu ya Tanzania kutokomeza ugonjwa wa Sotoka ya mbuzi na kondoo kwani ugonjwa huo umeendelea kusababisha hasara ya hadi dola bilioni 2.4 kila mwaka kwa bara la Africa hivyo kampeni ya kutokomeza PPR ifikapo 2030.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Dkt. Benezeth Lutege, alisema warsha hiyo ni tukio la kihistoria kwa sekta ya mifugo nchini Tanzania ikiwa ni sehemu muhimu ya kutokomeza ugonjwa wa Sotoka ya mbuzi na Kondoo kwani unaathiri afya ya mifugo na kukwamisha biashara.
Mwakilishi wa Shirima la Chakula na Kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) nchini Tanzania, Dkt. Justine Assenga ameipongeza Tanzania kwa hatua muhimu ya kuanisha mkakati wa kitaifa wa kutokomeza ugonjwa wa Sotoka ya mbuzi na Kondoo.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni