◼️Ataka TAFICO liwe Shirika la mfano
◼️Kamani awaita vijana kuchangamkia fursa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amezitaka mamlaka zilizopo chini ya Wizara yake kwa upande wa sekta ya Uvuvi kuwa makini kwenye ushirikishaji wa sekta binafsi za ndani na zile za nje.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo wakati wa ziara yake kwenye Ofisi za Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) aliyoifanya Disemba 05,2025 jijini Dar-es-salaam ambapo amelitaka shirika hilo kushirikisha sekta binafsi za ndani kwa mambo ambayo sekta hizo zinaweza kufanya kwenye mchakato wa kufufua shughuli zake unaoendelea hivi sasa.
“Hatuwezi kukwepa kabisa kushirikisha sekta binafsi za nje kwa sababu za uzoefu, teknolojia, mitaji na kupata masoko ya nje kwa sababu biashara hii ya mazao ya uvuvi ni kubwa hivyo soko likichangamka masoko ya ndani hayatatosha” Amesisitiza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ng’wasi Kamani amewataka vijana waliopo nje ya mfumo rasmi wa ajira kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya Uvuvi hususan zile zitakazotokana na shughuli za Shirika hilo pindi litakavyoanza kufanya kazi
“Nimefurahi kuona hapa wapo vijana ambao walichangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya Uvuvi mpaka wakaajiriwa hivyo niwaombe nyie muwe mabalozi kwa wenzenu waliopo nyumbani mkawaeleze fursa hizi zilizopo kwani ndio dhamira ya Mhe. Rais ya kuhakikisha vijana wananufaika na sekta hizi za uzalishaji” Amesema Mhe. Kamani.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu wake Mhe. Kamani wanatarajiwa kuendelea na ziara yao Disemba 05,2025 ambapo watatembelea Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) na Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU).





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni