Nav bar

Jumamosi, 6 Desemba 2025

NI JUKUMU LA KILA MTANZANIA KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI

 ◼️Apiga marufuku matumizi ya maneno “Uvuvi haramu”

◼️Asisitiza ni Uvuvi usiozingatia sheria na wanaofanya hivyo ni wahalifu

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally amepiga marufuku matumizi ya maneno “Uvuvi haramu” ambapo badala yake ametaka vitendo hivyo sasa vitambulike kama Uvuvi usiozingatia sheria na watu wanaofanya hivyo watambulike kama wahalifu.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo wakati akizungumza na watendaji na watumishi wa kitengo cha Uhifadhi wa Maeneo Tengefu alipofika kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kitengo hicho Disemba 06,2025 jijini Dar-es-salaam.

“Hakuna Uvuvi haramu, suala la uharamu na uhalali ni suala la Mwenyezi Mungu sasa mtu haramu maana yake aende motoni na sisi hapa duniani na Serikalini hatuna moto wa kupeleka watu wanaovua uvuvi haramu” Amesisitiza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa vitendo vya Uvuvi usiozingatia sheria vinatokana na kukosekana kwa utawala wa sheria katika sekta ya Uvuvi suala ambalo amesisitiza kuwa linapaswa kutekelezwa na kila Mtanzania.

“Kwa hiyo mimi sitakuwa na msamiati wa Uvuvi haramu kwa sababu Rais hajateua masheikh, mapadri, wachungaji au mitume bali ameteua Watanzania kusimamia sheria na kama sheria ni dhaifu bunge lipo na mimi ndo ninaiwakilisha sekta ya Uvuvi na Mifugo bungeni kwa hiyo tuimarishe sheria zetu” Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa kwa Watanzania popote walipo pindi wanaposhuhudia vitendo vinavyoashiria Uvuvi usiozingatia sheria wahakikishe wanawachukulia hatua za kisheria watu hao.

“We unamuona mtu ana nyavu za kihalifu, anavua kihalifu, wasimamizi wa sheria wanamlinda mhalifu afu wewe mwenye wajibu wa kusimamia utawala wa sheria unalalamika bila kuchukua hatua kwa hiyo hili ni tatizo letu sote na tutakapoanza kudhurika kutokana na uvuvi wa kihalifu tutaumia wote” Amehitimisha Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akisalimiana na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Uhifadhi wa MaeneoTengefu Bw. Godfrey Ngupula muda mfupi baada ya kufika kwenye ofisi za kitengo hicho Disemba 06,2025 jijini Dar-es-salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akisaini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kufika kwenye ofisi za kitengo cha Uhifadhi wa Maeneo Tengefu Disemba 06,2025 jijini Dar-es-salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara yake na watumishi wa kitengo cha Uhifadhi wa Maeneo Tengefu muda mfupi baada ya kuzungumza nao Disemba 06,2025 jijini Dar-es-salaam.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni