◼️Asisitiza Wafugaji ndio kipimo cha utendaji wao
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka Maafisa ugani nchini kujenga ushirikiano madhubuti baina yao na wafugaji utakaolenga kutoa taarifa sahihi, kuelimisha, kutoa ushauri wa kitaalam, kusambaza teknolojia na kupata mrejesho wa matumizi ya teknolojia hizo.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa maelekezo hayo wakati wa Hafla fupi ya kukabidhi pikipiki 381 kwa Maafisa ugani wote waliopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa iliyofanyika Disemba 04,2025 jijini Dar-es-Salaam ambapo amewataka kutanguliza dhana ya majadiliano zaidi badala ya kufundisha pindi wanapokuwa uwandani.
“Huduma za Ugani ni muhimu na ni kiungo kati ya watafiti na wafugaji ili kupata ufugaji wenye tija hivyo ni vema mkaimarisha mahusiano hayo kwa hiyo niwaombe na nirejee tena kama alivyoelekeza Mhe. Rais twendeni kuwahudumia watu sio kama tunawafundisha kama hawana taaluma au uelewa bali tukajadiliane nao na kuwasikiliza” Amesisitiza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amewataka maafisa ugani hao kuhakikisha wanatatua changamoto zote zinazowakabili wafugaji huku akiwataka kutoa taarifa kwa upande wa changamoto zinazopaswa kutatuliwa katika ngazi ya Wizara.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo kwa niaba ya Maafisa ugani nchini Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemhakikishia Mhe. Balozi Dkt. Bashiru kuwa pikipiki hizo zitatunzwa na kufanya kazi iliyokusudiwa.
“Nikuhakikishie Mhe. Waziri hutaziona pikipiki hizi zikitumika kama bodaboda na tutahakikisha kwamba vitendea kazi hivi vinaendelea kutumika kwenye zoezi la Chanjo za Mifugo na Utambuzi linaloendelea nchi nzima” Ameongeza Mhe. Prof. Shemdoe.
Akizungumza kwa Niaba ya Wakuu wa Mikoa Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa pikipiki hizo zitasaidia kuchochea ufugaji wa kisasa na kuwafanya wafugaji kukopesheka hatua ambayo itaboresha maisha yao na kuakisi dhana ya “Tabasamu” kupitia Wizara za Mifugo na Uvuvi na ile ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Nao wawakilishi wa Maafisa ugani Bw. Peter Shirima kutoka Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na Odetha Muchukuzi kutoka mkoani Dar-es-Salaam wameishukuru Serikali kwa kuwapatia nyenzo hizo ambazo wamesema kuwa zitawasaidia kuwahudumia wafugaji kwa urahisi zaidi.
Pikipiki hizo zinaifanya Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa imeshagawa jumla ya pikipiki 2581 hadi sasa ambazo zote zimelenga kuwarahisishia maafisa ugani hao kuwafikia wafugaji.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni