Nav bar

Jumatano, 1 Oktoba 2025

WAZIRI MKUU-KAZI WAONESHWA “KAZI” SHIMIWI

◼️Mifugo na Uvuvi yawatembezea kichapo cha magoli 2-0

Timu ya soka ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanzia ilipoishia kwenye michuano ya SHIMIWI inayoendelea jijini Mwanza baada ya kuitandika timu ya soka kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi magoli 2-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Sabasaba leo Septemba 02,2025.

Katika mchezo huo kikosi cha Mifugo na Uvuvi kilionesha kiu ya kuibuka na ushindi mapema baada ya kufanya mashambulizi ya nguvu kwenye lango la wapinzani wao na kufanikiwa kuandika bao la kwanza dakika ya 11 kupitia kwa mshambuliaji wao Valentino Kikoti “Jaja” ambaye alikuwa tishio kubwa kwa walinzi wa Waziri Mkuu-Kazi kwenye mchezo wa leo.

Goli hilo liliwaongezea ari wachezaji wa timu ya Mifugo na Uvuvi ambapo waliongeza kiwango cha mashambulizi langoni mwa wapinzani wao na kufanikiwa kutengeneza nafasi na kufunga magoli kadhaa yaliyokataliwa na mwamuzi kwa kile alichokotafsiri kuwa ilikuwa ni mipira ya kuotea.

Hata hivyo hilo halikukikatisha tamaa kikosi cha Mifugo na Uvuvi ambapo kiliendelea kuumiliki mchezo huo na kuongeza mashambulizi yaliyopelekea kupata bao la pili dakika ya 25 kipindi cha lililowekwa kimiani na winga wake wa kulia Deonatus Magendelo ambalo alilifunga baada ya kupokea pasi nzuri ya mwisho kutoka kwa mshambuliaji wa timu hiyo Valentino Kikoti.

Mara baada ya ushindi huo kikosi hicho sasa kitamenyana na timu ya soka ya TAKUKURU kwenye mchezo unaofuatia ambao utapigwa kwenye uwanja wa Nsumba jijini Mwanza.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni