Nav bar

Jumatatu, 11 Agosti 2025

MIFUGO NA UVUVI VINARA NANE NANE 2025!

Na. Omary Mtamike

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye maonesho ya kimataifa ya Nane Nane 2025 kwa upande wa Wizara za kisekta ikifuatiwa na Wizara ya Kilimo iliyoshika nafasi ya pili.

Wizara hiyo imeibuka na ushindi huo baada ya kuongoza katika vigezo mbalimbali hali iliyochagizwa na maandalizi mazuri iliyofanya katika maonesho hayo huku kivutio kikubwa kikiwa ni Paredi ya Mifugo iliyoambatana na maonesho ya Ndege nyuki maalum inayotumika kwenye udhibiti wa Uvuvi haramu.

Akizungumza katika kilele cha Maonesho hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mbali na kuipongeza Wizara hiyo kwa jitihada ilizochukua katika udhibiti wa magonjwa ya Mifugo kupitia utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, ameielekeza kuhakikisha inaweka kituo cha Ugani kwenye viwanja vya Maonesho hayo jijini Dodoma ambavyo rasmi leo vimetambulishwa kwa jina la Dkt. John Samwel Malecela ili wananchi waendelee kunufaika na elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemshukuru Rais Samia kwa kuiongezea Wizara yake bajeti kwa mwaka huu wa fedha ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo imeiongeza ajira kwa watu wengi hususan wanawake na vijana.

Maonesho hayo ambayo kilele chake ni Agosti 08 ya kila mwaka yataendelea kwa siku mbili zaidi kwa mwaka huu ili kuwapa fursa watu wengi zaidi kwenda kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akimuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba (kushoto) kuhusu kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mbari za Mifugo ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa nchini muda mfupi baada ya kufika kwenye banda hilo leo Agosti 08, 2025 kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Uzalishaji na Uendeleza wa Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael (kushoto) akimueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan namna Wizara inavyohakiki ubora wa mazao ya Mifugo na malisho muda mfupi baada ya Rais Samia kufika kwenye banda la Wizara hiyo leo Agosti 8, 2025 kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (kushoto) akimueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) maendeleo ya Utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo muda mfupi baada ya Rais Samia kufika kwenye banda la Wizara hiyo leo Agosti 8, 2025 kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni