Na. Hamis Hussein
Timu ya Watalam wa Udhibiti Ubora na Masoko ya Mazao ya Uvuvi (QC) na Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza utoaji wa elimu ya Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi, Uhifadhi bora wa Mazao ya Uvuvi na Umuhimu wa ulaji wa mazao ya Uvuvi kwa wadau wa sekta ya uvuvi Ukanda wa Ziwa Victoria ili kudhibiti uvuvi haramu na kulinda rasilimali zilizopo ndani ya ziwa hilo.
Timu hiyo ilianza utoaji elimu hiyo kwa wadau hususan Wavuvi na Wachakataji wa mazao ya uvuvi Agosti 23, 2025 katika mialo ya Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza mara baada ya kikao kazi cha kujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu ukanda wa Ziwa Victoria.
Akizungumza katika Mwalo wa Kayenze Kubwa uliopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza Afisa Uvuvi Mwandamizi Bw. Hamprey Tilla aliwahimiza wavuvi kufuata sheria za uvuvi na kuuunga mkono jitihada za serikali kwa kuwa mabalozi na wadau muhimu katika kutafuta mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu.
"Ndugu zangu sisi tunaongezeka lakini ziwa haliongezeki, tufuate sheria lakini sote kwa pamoja, nyie wavuvi, serikali na wadau wengine wote tunawajibu wa kulinda rasilimali hizi ndani ya ziwa letu"
Kwa upande wake Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Gedrude Migodela aliwahimiza wadau hao wa uvuvi juu umuhimu wa matumizi ya miundombinu bora ya kuhifadhia mazao ya Uvuvi ili yaweze kukidhi vigenzo vya kimaabara kabla ya kuingizwa sokoni.
"Ni muhimu tukatumia njia bora kuhifadhi mazao yetu kwa sababu mazao haya yakipelekwa maabara yakibainika kuwa na changamoto zitokanazo na uhifadhi wake yatakosa soko" alisema Bi Migodela.
Akiwa kwenye Mwalo wa Shadi Wilayani Nyamagana Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Kudhibiti na Kusimamia Rasilinali za Uvuvi (FRP) Mwanza Bw. Hamad Stima aliwahimiza wadau wa uvuvi katika eneo hilo juu ya umuhimu wa utunzaji wa rasiliamli za uvuvi kwa ajili kulinda uchumi na afya za wananchi.
Pia, timu hiyo iliwakumbusha na kuwahimiza wadau hao juu ya umuhimu wa ulaji wa mazao ya uvuvi ambapo Afisa Uvuvi Mwandamizi Bi. Grace Kakama alisema familia nyingi za wavuvi zimekuwa hatuzitumii mazao ya uvuvi kama sehemu ya chakula chao kwa ajili protini.
Baadhi ya Wavuvi waliuliza maswali mbalimbali wakati wakipokea elimu hiyo kutoka kwa wataalam wa wizara na kuiomba serikali kufanya sensa ya wavuvi wote nchini kujua idadi yao ili waweze kupangiwa maeneo maalum ya kufanya shughuli za uvuvi, kupunguza idadi ya boti ikiwa ni sehemu ya maoni yao kuhusu utunzaji wa rasilimali za Uvuvi kwenye ziwa hilo.
Zoezi la utiaji elimu hiyo linaendelea leo Agosti 24, 2025 kwa mialo iliyopo Wilaya Ukerewe kwa Mkoa wa Mwanza na kisha mialo ya Mkoa wa Mara na Simiyu.











Hakuna maoni:
Chapisha Maoni