Na, Hamisi Hussein, Rorya - MARA
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Kimansa Bugomba amesema ulinzi wa rasilimali za sekta ya uvuvi utasaidia kuongeza upatikanaji wa mazao ya uvuvi na kuchochea uchumi wa wananchi na pato la Taifa.
Akitoa elimu ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa ukanda wa Ziwa Victoria Agosti 26, 2025, kwa Wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi katika Mwalo wa Isegere uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara Bw. Bugomba amesema wajibu wa kulinda rasilimali za uvuvi ni jambo shirikishi baina ya wadau na serikali kutokana na umuhimu wake kiuchumi.
"Wizara yetu kwa mwaka 2025/2026 katika vipaumbele tulivyonavyo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi kwa kutumia teknolojia, ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi, kwa hiyo
sisi serikali na nyie wadau wa uvuvi tunawajibika kulinda rasilimali hizo ili sote tunufaike kiuchumi" alisema Bugomba.
Awali, akiwa Ofisini Kwake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfanis Ilekizemba aliiambia timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa sekta ya uvuvi inachangia shilingi bilioni 1.8 kwenye mapato ya halmashauri na kuahidi kuiunga mkono Wizara hiyo juu ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali hiyo.
"Tunashukuru Wizara kuendelea kuelimisha juu ya ulaji wa samaki kwa jamii zetu na sisi tutatoa ushirikiano kuanzia kwenye ulinzi wa rasilimali za Uvuvi, na kuhimiza watu wetu wale samaki".alisema Dkt. Ilekizemba.
Akiwa kwenye Mwalo huo wa Isegere Mfawidhi wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kituo cha Mkoa wa Mara Bw. Yohana Mirumbe aliwambia wavuvi, wamiliki wa vyombo vya uvuvi na wadau wote wanahusika katika mnyororo wa thaman wa sekta ya uvuvi kuzingatia sheria na taratibu za ukataji wa leseni na matumizi sahihi ya zana za uvuvi ili kuondokana na uvuvi haramu.
Alisema kuna baadhi ya wavuvi hutumia nyavu zinazoruhusiwa kisheria lakini wanazitumia kuvua maeneo yasiyoruhusiwa akitolea mfano kutumia wavu wa kuvulia dagaa kwenda kuvulia samaki aina ya Sangara akisisitiza kuwa ni kosa kisheria.
Naye Afisa Uvuvi Mkuu ambaye anasimamia udhibiti ubora na masoko (QC) mkoani Mara Bw. Mkinze Rajabu alielezea vigenzo vya ubora wa mazao ya uvuvi yanakidhi ushindani wa soko ambapo aliwaelimisha wadau wa uvuvi njia za kudhibiti ubora na jinsi ya kuongeza thaman ya Mazao ya Uvuvi.
Baadhi ya wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi katika mwalo huo wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa elimu hiyo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuiomba serikali kuongeza jitihada za ufutiliaji na usimamizi wa sheria za uvuvi ili kutokomeza uvuvi haramu katika ukanda wa Ziwa Victoria.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni