Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amewataka wafugaji nchini kuwa na mabadiliko ya kifikra ili waondokane na ufugaji wa kienyeji na kufanya ufugaji wa kibiashara na wenye tija.
Mhe. Ndaki Aliyasema hayo alipokuwa akizindua Baraza la Wataalamu wa Chama cha Wafugaji Tanzania lililofanyika jijini Dodoma Aprili 20, 2022.
Akiongea na wajumbe wa baraza hilo alisema dira ya chama cha wafugaji ni kuwa na ufugaji wenye tija na ufugaji wa kibiashara na hivyo aliwaomba viongozi kusaidia kuwaelimisha wafugaji kufuga kibiashara.
"Ni muhimu sana sisi wafugaji tusaidiane kwa kuambiana ukweli kuhusu ufugaji wa tija na tubadilishe fikra zetu ili wafugaji waone ufugaji ni mali, " alisisitiza Ndaki
"tunaposema tufuge kibiashara tunalenga soko la hapa ndani lakini pia na masoko ya nje, tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua masoko ya nje kama ya Oman, Uarabuni na Ubelgiji", aliongeza
Aidha, aliwatahadharisha wafugaji kote nchini kuwa mwaka huu kumekua na mvua za kusuasua hivyo hali ya malisho na maji itakuwa sio nzuri kwa mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Jeremia Wambura alisema zoezi la utambuzi wa mifugo kwa njia ya kieletroniki tayari limeanzaa katika mikoa mingi na kwamba Halmashauri zote zinaendelea na utambuzi huo wa mifugo.
Pia, Wambura alisema changamoto kubwa ya wafugaji ilikuwa ni majosho lakini aliishukuru serikali kwa kujitaidi kuwajengea majosho hayo kiasi cha kupungua kwa changamoto hiyo.
.png)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni