Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

BADO WAFUGAJI HAWAJANUFAIKA IPASAVYO- NZUNDA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa pamoja na jitihada kubwa zinazofanyika kwenye sekta ya mifugo nchini, bado jamii inayoshughulika na shughuli za ufugaji haijanufaika kikamilifu kutokana na jitihada hizo.


Nzunda ameyasema hayo leo (20.04.2022) wakati akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo ya sekta ya Mifugo kutoka Taasisi za Serikali na sekta binafsi uliofanyika kwenye hoteli ya Royal jijini Dodoma ambao moja ya ajenda zake kuu ilikuwa ni Mpango wa mabadiliko wa Sekta hiyo kwa mwaka 2022/2023 hadi 2026/2027.


Nzunda amebainisha kuwa wadau wengi waliopo kwenye sekta ya Mifugo hawana mipango jumuishi ambapo alitoa rai kwa wadau hao kuhakikisha mipango yao inagusa moja kwa moja shughuli za wafugaji.


" Wafugaji wengi wanalalamika kuwa wadau wanaojihusisha na sekta yao wanatumia rasilimali nyingi kwenye maeneo ambayo hayagusi moja kwa moja maslahi yao na bahati mbaya tunasemwa kuwa tunajishughulisha zaidi na "soft skills" na sio "hardware" hivyo ni lazima tujitathmini ili kuona ni kwa kiwango gani mipango yetu tunayoiandaa inagusa maisha ya wafugaji" Amesema Nzunda.


"Nichukue nafasi hii kuyashukuru mashirika ya kimataifa na taasisi zisizo za kiserikali ambazo zimejielekeza kutatua changamoto za wafugaji moja kwa moja na mengine tunaona yamejikita kwenye tasnia zetu za maziwa, malisho na kuboresha mbari za wanyama " Ameongeza Nzunda.


Nzunda amewataka wadau wote wanaokwamishwa na vikwazo mbalimbali kwenye jitihada zao za kutaka kuendeleza sekta ya Mifugo wafike ofisini kwake ili aweze kuwasaidia kutatua vikwazo hivyo.


"Upo usemi unaosema ukitaka kufika haraka tembea mwenyewe na ukitaka kufika mbali tembea na wenzio hivyo na sisi kama Serikali tupo tayari kutembea pamoja na wadau wote wa sekta ya Mifugo ili tuweze kufika mbali" Alihitimisha Nzunda.


Akiwasilisha mpango huo Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango (Mifugo) Bw. Mbaraka Stambuli amesema kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuimarisha sekta ya mifugo ili kuiwezesha kuwa na tija, kuchangia uchumi wa viwanda, kuimarisha biashara ya ndani na nje ya nchi na kunufaisha wananchi kwa ujumla.


"Utekelezaji wa mpango huu una maeneo 7 ya kimkakati ambayo yatatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 (2022/2023-2026/27) na miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, kuimarisha huduma za maji, malisho na vyakula vya mifugo na kuboresha huduma za ugani" Aliongeza Stambuli.


Kwa upande wake mmoja wa wadau walioshiriki mkutano huo ambaye ni mwakilishi kutoka Taasisi ya kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) Bw. Eliaman Lyatuu amesema kuwa Taasisi yao ipo tayari kuunga mkono jitihada za Serikali hasa kwenye eneo la utambuzi wa idadi ya mifugo kutumia mifumo ya TEHAMA na eneo la uboreshaji teknolojia ya uhimilishaji.


"Natambua kupitia mpango huu itatengenezwa kanzi data ambayo itatumika kufanya tathmini za shughuli mbalimbali za ufugaji hapa nchini hivyo nashauri kanzi data hiyo iwe kwenye lugha rahisi ambayo wafugaji wataielewa kwa urahisi" Aliongeza Lyatuu.


Zaidi ya shilingi Bilioni 1.9 zinatarajiwa kutumika kutekeleza jumla ya maeneo 7 ya kimkakati yaliyopo kwenye mpango huo wa miaka 5 ambao unatarajiwa kuwa suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo kwa sasa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixson Nzunda akifafanua mikakati ya Serikali inayolenga kuboresha sekta hiyo wakati akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo ya sekta ya Mifugo kutoka Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi uliofanyika kwenye hoteli ya Royal jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani (Sekta ya Mifugo), Dkt. Angelo Mwilawa (wa kwanza kulia) na baadhi ya wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiandika maelekezo yanayotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Bw. Tixson Nzunda (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo ya sekta hiyo uliofanyika kwenye hoteli ya Royal jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni