Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

​UDSM YAOMBWA KUJIKITA KWENYE TAFITI ZA UVUVI

Na Mbaraka Kambona,


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Chuo kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE) kimeombwa kufanya tafiti nyingi zinazohusiana na masuala ya sekta ya uvuvi ili kusaidia kutoa majawabu ya changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo hapa nchini.


Rai hiyo ilitolewa Aprili 14, 2022 jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Bi. Mary Mwangisa wakati wa kufunga warsha ya kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Uvuvi Mdogo na Ufugaji wa Viumbe Maji.


Wakati akifunga maadhimisho hayo ya siku tatu yaliyoanza Aprili 12-14, 2022, Bi. Mwangisa alimuomba Mkuu wa Chuo Kikuu kishiriki cha  Elimu cha Dar es Salaam (DUCE) ambao wameshirikiana na Wizara ya Mifugo na uvuvi kuandaa maadhimisho hayo chini ya ufadhili wa Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO), kuandaa utaratibu wa kukutana na wadau wa uvuvi ili kuendeleza sekta ya uvuvi.


“Tunakishukuru Chuo cha DUCE kwa ushirikiano wao na kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika, tunaomba mkutane na Wavuvi wetu ili kufanya maandiko mengi ya kuomba fedha kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi,” alisema Mwangisa


Aidha aliwataka washiriki wa maadhimisho hayo ambao wamepata ujuzi mbalimbali kwenda kusambaza elimu waliyoipata katika maeneo yao ili shughuli za uvuvi ziendelee kuwa na tija zaidi huku akiwasisitiza kuhakikisha wanafanya uvuvi endelevu kwa manufaa ya taifa.


“Naomba mkazingatie usimamizi wa rasilimali za uvuvi, kwa sababu msipokuwa na utawala bora wa kuhamasishana usimamizi mzuri wa rasilimali za uvuvi hakuna maendeleo yatakayopatikana katika sekta hii ya uvuvi,” aliongeza


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DUCE, ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Uvuvi Mdogo na Ufugaji wa Viumbe Maji, Prof. Stephen Maluke alisema wako tayari kutoa ushirikiano kwa wavuvi ili sekta ya uvuvi iendelee kutoa mchango mkubwa nchini.


“Pengine hata Wizara ya Mifugo na Uvuvi walikuwa hawafahamu kama sisi DUCE tuna watafiti wazuri wa masuala ya uvuvi na mifugo pia hasa katika upande wa mazingira na uchumi hivyo tupo tayari kushirikiana kwa sababu tuna wataalamu wa kutosha ambao watashirikiana na wavuvi ili kuendeleza sekta hii muhimu ya uvuvi,” alisema 


 Mchakato  wa kusherehekea mwaka wa Uvuvi mdogo na Ufugaji viumbe majini ulianza tangu mwaka 2016 ambapo wadau wa nchi mbalimbali za ukanda wa Carribean na Latin America walikutana na kuomba Umoja wa mataifa utangaze rasmi mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa uvuvi mdogo na ufugaji viumbe majini hususani samaki.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni