Na Mbaraka Kambona,
Wadau wa Sekta ya Uvuvi nchini kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) wamekutana kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Uvuvi Mdogo na Ufugaji wa Viumbe Maji.
Akifungua maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam Aprili 12, 2022, Mkurugenzi Msaidizi, Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko, Bw. Stephen Lukanga alisema kuwa mchakato wa kusherehekea mwaka wa Uvuvi mdogo na Ufugaji viumbe majini ulianza tangu mwaka 2016 ambapo wadau wa nchi mbalimbali za ukanda wa Carribean na Latin America walikutana na kuomba Umoja wa mataifa utangaze rasmi mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa Uvuvi mdogo na ufugaji viumbe majini hususani samaki.
“Sekta ya uvuvi imebeba watu wengi hapa kwetu Tanzania ambapo inakadiriwa watu wapatao laki mbili na elfu tano (205,000) ni wavuvi wadogo wanaojishughulisha moja kwa moja na shughuli za uvuvi na watu zaidi ya milioni nne wanajishughulisha na uchakataji wa mazao ya uvuvi”, alisema Lukanga
Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua kadha wa kadha katika kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uvuvi hususan uhaba wa mitaji na matumizi ya zana duni za uvuvi.
Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inatambua mchango na changamoto wanazokabiliana nazo wavuvi wadogo na ndio maana inawahamasisha wajiunge katika vyama vya ushirika ili serikali iweze kuwawezesha mikopo na waweze kuinua uvuvi wao.
“Serikali pia inawawezesha wachakataji wa mazao ya uvuvi kwa kuwapa teknolojia nyepesi na za kisasa pamoja na zana bora za uvuvi ili waweze kuandaa mazao yao kwa ubora unaokubalika ndani na nje ya nchi”, alifafanua
Naye Mratibu wa Mradi wa Uvuvi mdogo, Lilian Ibengwe alisema kuwa wamekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi na watapitia tafiti mbalimbali zilizokuwa zimeshafanyika hapa nchini na kuona ni namna gani tafiti hizo sasa zinakwenda kutumika kutatua changamoto za wavuvi wadogo.
Aliongeza kwa kusema kuwa mwaka huu wa IYAFA unalenga kuwakumbusha juu ya umuhimu wa sekta ya uvuvi mdogo na kuongeza kasi ya kutatua matatizo yanayojitokeza katika sekta ya uvuvi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni