Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda, amewambia watalaam wa uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo kanda ya kaskazini (ZVC) na Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuwa tafiti zote wanazofanya za uchunguzi wa magonjwa ya Mifugo wahakikishe zinawafikia wafugaji ili zifanyiwe kazi na wahusika ili Sekta ya Mifugo iweze kuwa na tija kwa taifa.
Hayo ameyasema leo tarehe 11 Aprili 2022 alipofanya ziara ya kikazi TVLA, ZVC,kituo cha Taifa cha uzalishaji Mifugo kwa njia Chupa (NIC) na Wakala ya vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Kampasi Tengeru (LITA) mkoani Arusha.
"Fanyieni kazi na matokeo ya tafiti za Magonjwa ya Mifugo Mhakikishe zinawafikia wafugaji, Lakini pia toeni taarifa hizo za tafiti kwa Serikali kwa maana ya Sekretarieti ya Mkoa, Serikali za Mitaa na pia ombeni nafasi kwenye vikao vya RCC, DCC na Mabaraza ya madiwani ili kuwasilisha hizo tafiti zenu, lengo ikiwa ni kujenga uelewa na kuwashawishi watoa Maamuzi". Alisema Nzunda.
Aidha, Bw. Nzunda amewataka wataalam hao kuhakikisha wanaongeza juhudi katika kuwaelimisha wafugaji kuchanja na kuogesha Mifugo yao, akisema kuwa tafiti zinaonyesha asilimia 70% ya Magonjwa anayougua binadamu yanatoka kwa kwa wanyama, kwahiyo amewataka watalaam hao kutumia Sheria, kanuni na Sera kuhakikisha wafugaji wanachanja Mifugo yao ili kuzuia Magonjwa hayo.
Pia Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) amesema kuwa Tanzania ina ng'ombe takribani 33.9 ambayo ni nchi ya pili Africa kuwa na Mifugo Mingi, lakini Mifugo hiyo haina tija kwa taifa kwani inachangia asilimia 7.1 tu katika pato la Taifa, ambapo ametoa mfano kuwa Tanzania inazidiwa na nchi kama Botswana yenye Mifugo Milioni mbili tu lakini mchango wake katika pato la taifa ni Mkubwa sana.
Pia Bw.Nzunda amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii, kujituma, weledi na uadilifu, na kuelekeza kwamba kwa mwaka fedha 2022/23 Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) itaanza kutekeleza mpango wa Mkataba wa kazi (Performance Cotract) ili kupima utendaji kazi wa Kila mtumishi na kuhakikisha anafikia malengo aliyopangiwa.
Vilevile, Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mufugo) imeandaa Mpango Mkakati wa Kubadilisha Sekta ya Mifugo ambao una maeneo makuu saba ya kimkakati ambayo ni pamoja na: Kuwezesha Upatikanaji wa Mbegu bora za Mifugo, Kuimarisha huduma za Maji, Malisho na vyakula vya Mifugo, kuimarisha afya za Mifugo na Kuboresha huduma za Ugani.
Maeneo Mengine ya kimkakati ni, kuimarisha huduma za Utafiti na Mafunzo ya taaluma za Mifugo, kuwezesha uongezaji thamani mazao ya Mifugo na kuimarisha Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Mifugo amewapongeza wakala ya vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kampasi ya Tengeru kwa kuwa na shamba kubwa la hekta 42 za malisho na kuwata kuongeza uzalishaji wa Malisho na Mbegu za malisho na pia kuwaelekeza kuanzisha Duka la mbegu za malisho kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na Idara ya Uendelezaji nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo.
Akiwa LITA Kampasi ya Tengeru Katibu Mkuu Mifugo alipata fursa ya kutembelea baadhi ya Miradi inayoendelea kutekelezwa chuoni hapo, kama Ujenzi wa Madarasa Manne ya Wanafunzi yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 120 kwa wakati Mmoja kila Darasa pamoja na Maabara ya kisasa.
Wakati huo huo katibu Mkuu alipata fursa ya kukagua utendaji kazi wa kituo cha Taifa cha Uzalishaji Mifugo kwa njia chupa (NAIC) na kuridhika na kazi zinazofanyika kituoni hapo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni