Nav bar

Jumatatu, 9 Mei 2022

WATUMISHI SEKTA YA UVUVI WAFANYA KIKAO KUBORESHA UTENDAJI KAZI WAO

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi wamefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa ajili ya kujadili namna walivyotekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022 na kujipanga kutekeleza bajeti ya mwaka 2022/2023.

 

Kikao hicho kimefanyika (12.04.2022) Mkoani Singida ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amewasihi watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuona ni namna gani wanaweza kutatua changamoto zilizopo ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi kwenye pato la taifa.

 

Dkt. Tamatamah amesema kikao hicho ni muhimu kwa watumishi kwa kuwa watumishi wanashirikishwa kwa uwazi kuhusu namna walivyotekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022 na kujipanga kutekeleza bajeti ya mwaka 2022/2023.

 

Aidha, amewasihi wajumbe wa walioshiriki baraza hilo kuhakikisha wanatoa ushauri mzuri ili kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa.

 

Pia, amewataka watumishi kuendelea kujilinda na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza na kuwataka watumishi kufanya mazoezi ili kuendelea kuimarisha afya zao.

 

Katibu mkuu huyo amewapongeza wafanyakazi wa Sekta ya Uvuvi kwa kushiriki vyema kwenye mashindano ya (SHIMIWI), hivyo kuhakikisha wanaendelea kujiandaa ili katika mashindano yanayofuata wanafanya vizuri zaidi.

 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala amesema kikao hicho kimewasaidia kujua changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo katika utekelezaji wa bajeti na hivyo kuandaa mikakati ya kukabiliana nazo.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi - Utumishi, Bi. Mary Mwangisa amesema kuwa watumishi wanapata elimu ya kuwasaidia kwenda kuboresha utendaji kazi wao kwa kuwa watakuwa wameshafahamu kazi zinazotakiwa kutekelezwa kulingana na bajeti iliyotengwa.

 

Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Bi. Jane Kisanga amesema kuwa watumishi wamefarijika sana kushiriki kwenye kikao hicho ambacho kimewasaidia kuzitambua changamoto wanazokabiliana nazo na kujadili namna zinavyoweza kutatuliwa ili kuhakikisha sekta inaendelea kukua na kuchangia katika pato la taifa.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni