Nav bar

Jumamosi, 24 Julai 2021

SERIKALI KUKARABATI SOKO LA KIMATAIFA SAMAKI LA FERI

Mradi wa ukarabati wa soko la kimataifa la Samaki la Feri umepangwa kutekelezwa kwa muda wa miezi saba bila kuathiri shughuli za wafanyabiashara na wavuvi.

 

Hayo yamesemwa leo (04.07.2021) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kwenye mkutano na wafanyabiashara na wavuvi wa soko la kimataifa la samaki la feri jijini Dar es Salaam uliokuwa na lengo la kuwaelimisha kuhusu nia ya serikali kufanya ukarabati katika soko hilo.

 

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Ndaki amesema kuwa Wizara yake imeandaa mpango wa uhamishaji wa watu kwa muda katika maeneo ya soko yatakayofanyiwa ukarabati kabla ya kuhamishiwa.

 

“Wafanyabiashara katika kanda 1 na 2 watatambuliwa na kuhamishiwa maeneo ya muda yaliyoandaliwa. Mpango huu utahakikisha kuwa baada ya ukarabati wafanyabiashara waliohamishwa watarudishwa katika maeneo yao ya awali”. Amesema Waziri Ndaki.

 

"Lengo ni kuhakikisha tunawawezesha wavuvi kuongeza ufanisi na tija katika kazi yao sambamba na kuongeza mchango wao katika pato la Taifa, mwaka 2021 pato la Taifa ilikuwa ni asilimia 1.7, tunakusudia siku zijazo pato hili likue" aliongeza Waziri Ndaki.

 

Aidha Waziri Ndaki amesema miundombinu ya uvuvi hususan mialo na masokoni ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mazao ya uvuvi yanakuwa bora na salama kwa ajili ya afya ya walaji na hivyo kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.

 

Amesema miundombinu ya uvuvi inasaidia katika kudhibiti uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi, ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya Serikali na upatikanaji wa takwimu na taarifa sahihi za uvuvi.

 

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Rais Samia Hassan amejipanga kuhakikisha uzalishaji wa samaki na mazao yake unaongezeka na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi kwenye pato la taifa.

 

Naibu Waziri Ulega amesema serikali imepanga kununua meli kubwa ambazo zitakuwa zinafanya shughuli za uvuvi kwenye bahari kuu. Pia serikali itaweka miamba ambayo sio ya asili kwenye maeneo ya bahari ambayo itatumika kama maeneo ya mazalia ya Samaki.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anaeshuhulikia sekta ya uvuvi, Dkt.Rashid Tamatamah amesema kuwa soko hilo limeweza kutoa ajira rasmi zipatazo 117 na ajira zisizo rasmi takribani 2,780 hata hivyo soko hilo limekuwa na watumiaji 10,000 kwa siku wakati uwezo wa soko ni kuhudumia watu 1,500 kwa siku hivyo ni muhimu soko hilo kukarabatiwa.

 

Vilevile amesema kuwa mapato yatokanayo na soko la Feri ni kati ya Shilingi Milioni 135 hadi 150 kwa mwezi kutegemeana na hali ya uvuvi kwa mwezi husika.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wakuu wa Wilaya za Kigamboni na Ilala wamesema kuwa ukarabati wa soko hilo ni muhimu sana kwani ni moja ya chanzo kikubwa cha mapato kwa wafanyabiashara, wavuvi na serikali.

 

Serikali inatarajia kutumia kiasi cha zaidi ya Sh Bilioni 3.7 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa mialo na masoko kwa kuweka miundombinu mbalimbali ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kupunguza upotevu baada ya kuvunwa. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wafanyabiashara na wavuvi kuhusu nia ya serikali kufanya ukarabati wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo utaratibu maalum wa kuendelea na biashara umeandaliwa na usajili wa wafanyabiashara hao utafanyika kabla ya zoezi hilo ili kuhakikisha wenye kustahili wasipoteze nafasi zao mara baada ya ukarabati kukamilika. (04.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo aliwaeleza kuwa Mhe. Rais Samia Hassan amejipanga kuhakikisha uzalishaji wa Samaki na mazao yake unaongezeka na kuimarisha uchumi wa wadau wa sekta hiyo na pato la taifa kwa ujumla. (04.07.2021)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa taarifa fupi kuhusu hatua zitakazofuatwa katika ukarabati wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa miundombinu iliyopo katika soko hilo ina uwezo wa kuwahudumia watu 1,500 kwa siku lakini kwa sasa watu wanaopata huduma ni zaidi ya 10,000 hivyo ni muhimu soko hilo likarabatiwe. (04.07.2021)

Mbunge wa Jumbo la Ilala, Mhe. Mussa Zungu akizungumza kwenye Mkutano wa wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam. (04.07.2021)

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni. Mhe. Fatma Nyangasa akizungumza na wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo ameahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha ukarabati huo unafanyika na kukamilika ndani ya muda uliopangwa. (04.07.2021)


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng’wilabuza Ludigija akizungumza wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo ameishukuru wizara kwa uamuzi iliyochukua kukarabati soko hilo. (04.07.2021)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akikagua miundombinu ya soko la Feri kabla ya kufanya mkutano na wafanyabiashara na wavuvi juu ya hatua zitakazofuatwa katika ukarabati wa soko la samaki la Feri Jijini Dar es Salaam. (04.07.2021)


Wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri wakifuatilia Mkutano wa kuwaelimisha kuhusu hatua zitakazofuatwa katika ukarabati wa soko hilo uliofanyika Jijini Dar es Salaam. (04.07.2021)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni