Nav bar

Jumamosi, 14 Novemba 2020

NI MARUFUKU KULISHA MIFUGO VYAKULA VIBOVU - SERIKALI.

Serikali imepiga marufuku matumizi ya vyakula vilivyopoteza ubora wa kutumiwa na binadamu na kutumiwa kama vyakula vya mifugo kabla ya kuthibitishwa kwanza na wataalam wa maabara ya mifugo.

 

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

 

"Kumekuwa na mazoea ya vyakula ambavyo vimeshapoteza ubora wa matumizi ya binadamu kutumika kama vyakula vya mifugo hivyo ninapenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wafugaji, wazalishaji na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na uzalishaji wa vyakula vya binadamu kuwa ni marufuku kutumia vyakula hivyo bila Wizara yenye dhamana kuwa na taarifa na kujiridhisha kitaalam kama chakula hicho kinafaa au la," Amesisitiza Dkt. Rwiguza.

 

Aidha, Dkt. Rwiguza amebainisha madhara yanayoweza kumpata mtu ambaye atatumia mazao ya mfugo uliokula vyakula hivyo kuwa ni pamoja na kupatwa na magonjwa mbalimbali kama vile Kansa.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bw. Roggers Shengoto amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwasababu zaidi ya asilimia 90 ya wataalam walioalikwa walishiriki.

 

"Pia kupitia mafunzo haya tumegundua kuwa bado kuna haja ya Halmashauri za vijiji kutenga maeneo ya malisho ya mifugo na pia wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo bado hawazingatii sheria na kanuni za kufanya shughuli hizo, hivyo tuna imani wataalam hawa wataenda kuleta mabadiliko katika maeneo yote yenye changamoto kwa wafugaji" Ameongeza Shengoto.

 

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa wamenufaika na yote waliyofundishwa ambapo wameahidi kuyafanyia kazi na kubadilisha utendaji wao pindi wakirejea kwenye vituo vyao vya kazi.

 

"Kwa mfano, zamani nilikuwa naenda kwa mdau kama Mkaguzi na nilikuwa natumia lugha ya mamlaka lakini kupitia mafunzo haya nimefundishwa kumfuata mdau kama rafiki na kuzungumza naye kwa lugha ya kawaida" Amesema mmoja wa washiriki Veronica Ngoso.

 

Takribani wakaguzi 129 nchi nzima wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni.



Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akifafanua jambo mbele ya wataalam wa ukaguzi wa malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye kiwanda cha kusindika chakula cha mifugo kinachojulikana kama "Musoma Animal Feed" kilichopo mkoani Mwanza. (13.11.2020)



Meneja wa Kiwanda cha "Musoma Animal Feed", Bi. Maajabu Musa (mwenye kilemba cheusi) akitoa maelekezo ya namna chakula cha mifugo kinavyotengenezwa kiwandani hapo mbele ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Arusha, Shinyanga na Arusha wakati walipotembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Mwanza. (13.11.2020)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni