Nav bar

Jumapili, 15 Novemba 2020

SERIKALI KUIMARISHA UVUVI WA BAHARI KUU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.  John Pombe Joseph Magufuli amesema kuwa katika kipindi cha miaka 5 ijayo ya awamu yake ya pili ya uongozi atahakikisha sekta ya uvuvi inakuzwa ikiwemo kuimarisha shughuli za uvuvi wa bahari kuu kwa kununua Meli nane (8) zitakazofanya kazi katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ulioko Visiwani Zanzibar na Tanzania bara.


Dkt. Magufuli aliyasema hayo wakati akitoa hotuba yake ya kulifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma Novemba 13, 2020.


Wakati akilihutubia bunge hilo lililosheheni Wabunge wengi wapya, Dkt. Magufuli alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa shughuli za uvuvi ikiwemo Mito, Bahari na Maziwa hali ambayo inaifanya sekta ya uvuvi kuwa na nafasi kubwa ya kutoa mchango katika kukuza pato la taifa, kupambana na umasikini na tatizo la ajira.


Alisema pamoja na fursa hiyo iliyopo nchini bado mpaka sasa mchango wa sekta ya uvuvi upo chini hivyo serikali imekusudia kuwekeza nguvu zaidi ili kukuza sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.


"Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2018 ya  Kamati ya Bunge kuhusu shughuli za uvuvi wa bahari kuu, kama uvuvi wa bahari kuu utasimamiwa vizuri tunaweza kuiingizia serikali mapato ya moja kwa moja ya  shilingi bilioni 352.1 kwa mwaka," alisema Dkt. Magufuli


Aliendelea kueleza kuwa kufuatia hali hiyo serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itahakikisha  inasimamia mfumo mzima ikiwemo udhibiti wa shughuli za uvuvi ili malighafi itayokuwa inapatikana iweze kuchakatwa hapa nchini kwa lengo la kukuza thamani ya mazao ya baharini.


"Kwa bahati nzuri tumetunga sheria mpya ya kuendeleza shughuli za uvuvi nchini hivyo itasaidia katika usimamizi wa shughuli za uvuvi," alieleza Dkt. Magufuli


Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali kwa kushirikiana na  Shirika la Kimataifa la kuendeleza Kilimo (IFAD), itanunua Meli nane (8) za uvuvi katika bahari kuu ambapo 4 zitakuwa zikifanya shughuli zake Visiwani Zanzibar na 4 nyingine zitafanya shughuli zake katika ukanda wa pwani wa bahari ya hindi upande Tanzania bara.


"Kama mnavyofahamu suala la uvuvi ni la Muungano, tunakusudia kujenga bandari kubwa ya uvuvi itakayotoa ajira elfu thelathini (30,000) na tutaendelea kuhamasisha sekta binafsi kujenga Viwanda vya kuchakata samaki, sambamba na hilo tutakuza shughuli kwenye maziwa yetu makuu yaani Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika," alisisitiza Dkt. Magufuli


Aidha, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya uongozi wake serikali itahamasisha wavuvi wadogo wadogo kujiunga katika vikundi ili waweze kuwapatia mitaji, vifaa, ujuzi na zana za uvuvi.


"Tutapitia upya tozo ili kuwapunguzia wavuvi kero na kuvutia uwekezaji kwa wavuvi wetu," alifafanua Dkt. Magufuli


Kuhusu ujenzi wa Mabwawa, Dkt. Magufuli alisema kuwa watahamasisha watu binafsi kujenga mabwawa na kufuga kisasa kwa kutumia vizimba huku akisisitiza kuwa sekta ya uvuvi ni lazima itoe mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na hivyo kuwataka wateule wote wa sekta hiyo kuhakikisha wanasimamia vyema shughuli za uvuvi nchini.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni