Nav bar

Ijumaa, 13 Novemba 2020

WAFUGAJI WAKIJENGEWA UWEZO WATAKUZA UCHUMI WA TAIFA - MONGELA.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela amesifu juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha wafugaji wake wanafanya shughuli hiyo kwa tija na kwa kuzingatia dhana ya ukuzaji wa uchumi wao.

 

Mhe. Mongela ameyasema hayo leo (12.11.2020) baada ya kupokea timu ya wataalam wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo (Wizara ya Mifugo na Uvuvi) ambao wamefika mkoani humo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya siku mbili kwa wakaguzi wa vyakula vya mifugo kuhusu ukaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo

 

"Tunajitahidi sana kukuza tasnia ya ufugaji lakini uwepo mafunzo kama haya unawafanya wafugaji wetu wasiishie tu kufuga bali wafuge kwa tija na kukuza uchumi wao" amesema Mhe. Mongela.

 

Mhe. Mongela ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea na jitihada hizo za kujenga uwezo kwa wafugaji ili kuwafanya kuwa wafugaji bora wenye uelewa na ujuzi wa ufugaji wa kisasa badala ya ufugaji wa asili ambao haukuwa na tija kwa mfugaji pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mifugo.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza amesema kuwa wakaguzi hao ni sehemu ya wakaguzi 129 walioteuliwa kutoka kwenye Halmashauri na Sekretarieti za mikoa hapa nchini ambao baada ya kupatiwa mafunzo hayo watawawezesha wafugaji waliopo kwenye maeneo yao elimu kuhusu chakula bora cha mifugo ili waweze kuiboresha na kuongeza tija zaidi kwenye tasnia hiyo.

 

"Semina hii ni muhimu sana hivyo ninaomba tushirikiane na kwa sababu ninafahamu kuwa wote mna ujuzi hivyo leo tupo hapa kwa ajili ya kuongezeana uwezo wa kuwahudumia vizuri wafugaji wetu hasa ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 70 ya mahitaji ya mfugo ni chakula" Ameongeza Dkt. Rwiguza

 

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel ni ya awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza ilifanyika mkoani Morogoro na kuhusisha Mikoa ya Dar-es-Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga na Dodoma.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndg. Emanuel Tutuba (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Arusha muda mfupi kabla ya wataalam hao kupatiwa mafunzo juu ya ukaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza na kushoto kwake ni Katibu Tawala Msaidizi – Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Ndg. Emil Kasagala. (12.11.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela (kushoto) kuhusu Mafunzo ya siku mbiliWakaguzi wa Vyakula vya Mifugo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa, Ndg. Emanuel Tutuba. (12.11.2020)

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela (katikati) akifafanua juu ya namna mkoa huo unavyozipa kipaumbele sekta za Mifugo na Uvuvi mbele ya timu ya wataalam wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliofika Ofisini kwake kabla ya kuanza mafunzo kwa Wakaguzi wa Vyakula vya Mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Arusha yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. (12.11.2020)

Sehemu ya Wakaguzi wa Vyakula vya Mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Arusha wakifuatilia kwa umakini mafunzo yanayoendelea kuhusu ukaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni timu ya wataalam kutoka Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo (Wizara ya Mifugo na Uvuvi). (12.11.2020)

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Bw. Roggers Shengoto akiwasilisha mada ya sheria na kanuni za Maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo wakati wa mafunzo kwa wakaguzi wa vyakula vya mifugo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. (12.11.2020)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni