Nav bar

Jumatatu, 17 Agosti 2020

HALMASHAURI ZATAKIWA KUWEKA MPANGO MKAKATI WA WA MASOKO YA MAZAO YA MIFUGO

Halmashauri nchini zatakiwa kuwa na mpango mkakati wa masoko ya mazao ya mifugo ili kuhakikisha kunakuwa na ufugaji wenye tija.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel wakati alipofanya ziara ya kikazi Ikwiriri Wilayani Rufiji ambapo alizungumza na uongozi wa wilaya, wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata na vijiji, viongozi wa chama cha wafugaji na wakulima, na pia alitembelea moja ya eneo la linalotumika kulishia mifugo.

Prof. Gabriel amesema kuwa wizara inahamasisha ufugaji wa kisasa ambapo wafugaji wanahamasishwa kutumia mbegu bora kwa njia ya kutumia madume bora, uhimilishaji pamoja na njia ya upandikizaji wa viini tete.

“Wizara tunaendelea kuhamasisha ufugaji wa kisasa ambao utawafanya wafugaji wetu kuwa na mifugo michache itakayowaletea tija kubwa na kuongeza mapato ya serikali, ila ili kufanikisha hilo ni lazima halmashauri ziwe na mpango mkakati wa masoko ya mifugo na mazao yake ili mfugaji aone nia njema ya serikali katika kumbadilisha kutoka katika ufugaji wa asili”, alisema Prof. Gabriel.

Vilevile amezitaka halmashauri nchini kutumia Dawati la Sekta Binafsi katika kutengeneza maandiko mbalimbali ya vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu yanayohusu sekta ya mifugo na uvuvi ili waweze kupata mikopo kwa kuanzia kwenye mikopo inayotokana na asilimia kumi ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Katika kuhakikisha maendeleo ya sekta ya mifugo yanakuwa endelevu, Prof. Gabriel amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rufiji, Rashid Salum kwa kutenga na kutoa asilimia 15 ya makusanyo ya mapato yanayotokana na mifugo kwa ajili ya kuendeleza sekta ya mifugo. Hata hivyo, amewataka wakurugenzi wote nchini chini ya usimamizi wa Makatibu Tawala Mikoa kuhakikisha wanatenga fedha hizo na wanazitumia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya mifugo.

Pia katika kuhamasisha ufugaji wa ng’ombe bora wenye uwezo wa kutoa maziwa mengi na nyama bora, Prof. Gabriel ameahidi kutoa dozi za mbegu za uhimilishaji 1000 kwa ajili ya wilaya ya Rufiji. Vilevile ameahidi kuwaletea vifaranga vya kuku endapo halmashauri itafanya uhamasishaji katika vikundi.

Aidha, amewaahidi kuwa, kuhusu tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji ambalo wananchi walimueleza Mhe. Rais Magufuli, tayari imeshaundwa timu ya wataalam kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya TAMISEMI na ambayo itafika wilayani Rufiji kwa ajili ya kazi hiyo.

Prof. Gabriel amewataka viongozi wa chama cha wafugaji kuhakikisha wanakuwa karibu na wafugaji kwa kutambua changamoto wanazokutana nazo na kutoa taarifa sahihi kwa usahihi na kwa wakati. Wizara itahakikisha wafugaji hawaonewi lakini pia itasimamia kuhakikisha wafugaji wanatimiza wajibu wao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Pia amezitaka Halmashauri nchini kupitia serikali za vijiji kuhakikisha wanakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambayo itasaidia sana katika kupunguza kama sio kundoa migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Naye Katibu wa Chama cha Wafugaji Kibiti na Rufiji, Masanja Lukas ameishukuru serikali ya wilaya kwa namna wanavyowapa ushirikiano na kuomba wizara pamoja na mamlaka ya wilaya kuhakikisha wanasimamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji hayaingiliwi na watumiaji wengine wa ardhi pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo. Kwa kufanya hivyo migogoro hakutakuwepo na migogoro ya ardhi kwa kuwa sheria itakuwa inasimamiwa kuhakikisha kila mtu anapata haki yake.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Msafiri Msafiri ameishukuru wizara ya mifugo kwa ushirikiano mkubwa wanaopata ambapo wizara imetoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa majosho, minada, dozi za mbegu za uhilimishaji, na vifaranga vya kuku. Bw. Msafiri ameahidi kuwa, mkoa wa Pwani utasimamia na kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu Gabriel.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akimsikiliza Katibu wa Chama cha Wafugaji Kibiti na Rufiji wakati alipotembelea Ikwiriri kwa ajili ya kukagua maendeleo ya shughuli za Sekta ya Mifugo. (03.08.2020) 


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na viongozi na wataalam wa wilaya ya Rufiji pamoja na baadhi ya wenyeviti wa vijiji na viongozi wa chama cha wafugaji wakati alipotembelea Ikwiriri kwa ajili ya kukagua maendeleo ya shughuli za Sekta ya Mifugo. (03.08.2020) 


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akimkamata kondoo aliowakuta kwenye moja ya eneo linalotumika kulishia mifugo wakati alipotembelea Ikwiriri kwa ajili ya kukagua maendeleo ya shughuli za Sekta ya Mifugo. (03.08.2020

 


Picha ya pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel na Viongozi na wataalam katika wilaya ya Rufiji wakati alipotembelea Ikwiriri kwa ajili ya kukagua maendeleo ya shughuli za Sekta ya Mifugo. (03.08.2020) 

 


 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa ameshikilia kondoo aliyemkamata kwenye moja ya eneo linalotumika kulishia mifugo wakati alipotembelea Ikwiriri kwa ajili ya kukagua maendeleo ya shughuli za Sekta ya Mifugo. (03.08.2020) 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni