Nav bar

Jumatatu, 13 Mei 2019

NORWAY YAISAIDIA SEKTA YA UVUVI NCHINI



SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la NORAD, Norway imesaini mkataba wa uzalishaji samaki aina ya Sato zaidi ya tani 100,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mradi huo kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi,  mhe.Luhaga Joelson Mpina, Katibu Mkuu wa sekta ya Uvuvi  Dk. Rashid Tamatamah amesema,  mradi huo umekuja muda muafaka wakati nchi ina mahitaji makubwa.

Amesema lengo la Serikali ni kuzalisha samaki kwa wingi ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwenye mabwawa.

Amesema mradi huo umekuja kwa sababu ya kazi nzuri ya asasi ya Norges Vel, Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 20 sasa Tanzania imekuwa haifanyi vizuri katika sekta ya uvuvi ambapo imekuwa ikizalisha samaki tani 350,000 hadi 380,000 kwa mwaka."Samaki wanaozalishwa hivi sasa kwenye vyanzo vya maji idadi yake imebaki kuwa vilevile haiongezeki kwa kasi hivyo kuna kila haja ya kuongeza kasi ya uzalishaji,"alisema Tamatamah.

Amesema serikali ina nia ya dhati katika kuendeleza ufugaji samaki japokuwa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa.Tamatamah amesema fursa zilizopo hapa nchini ni pamoja na vyanzo vya vya maji, hali ya hewa na mazingira lakini wameshindwa kuzalisha tani za kutosha.

Amesema hadi sasa Tanzania imekuwa ikizalisha tani 16,000 wakati Norway inazalisha tani milioni 2.5 kwa mwaka."Hii ni fursa kwetu kwakuwa wenzetu wana ujuzi wa uzalishaji samaki, itasaidia kutuongezea ujuzi na sisi,"alisema Tamatamah.

Alibainisha kuwa Mradi huo utatekelezwa Kibaha mkoani Pwani ambapo vijana watapata fursa ya elimu pamoja na kuzalisha samaki.

Amesema anaamini hakuna uzoefu mbadala kwa mbinu hiyo kwani ni moja ya njia sahihi ya kupata ujuzi. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alisema mradi huo ni fursa na neema kwa wananchi wa Kibaha.

Alisema anaamini mradi huo utaongeza idadi ya samaki wanaozalishwa nchini pamoja naa kukuza uchumi wa nchi.

Naye, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Elizabeth Jacobson alisema, ana imani mradi huo utafungua fursa kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema mradi huo umeletwa ili kutokomeza changamoto zilizopo za uhaba wa samaki pamoja na kufungua njia za ujasiriamali kwa wananchi.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashidi Tamatamah, akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Joelson Mpina kwenye hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Ufugaji wa Samaki iliyofanyika katika ofisi za Wizara jijini Dr es salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni