Nav bar

Jumatano, 31 Oktoba 2018

SERIKALI IPIME MAENEO YA WAFUGAJI ILI WAMILIKISHWE KISHERIA




Wafugaji wa Halimashauri ya Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro wamewalalamikia watendaji wa Serikali na kwamba wao ndio wanao chochea Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Malalamiko hayo yametolewa jana na wafugaji wa kijiji cha Sanya Station, katika kata ya Kia, katika Halmashauri ya Wilaya Hai, walipokuwa wakitoa kero zao kwa Katibu Mkuu Mifugo, Prof.Elisante Ole Gabriel, aliyefika katika kijiji hicho kusikiliza kero za wafugaji hao kwa Niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe .Luhaga Joelson Mpina.

“Sisi Wafugaji na Wakulima natuna tatizo kabisa, Shida kubwa iko kwa hao Mgambo, ambao wanatumwa na watendaji wa Serikali waje wakamate Ngombe wetu bila kosa lolote na kufanya mradi wao wa kuwaingizia fedha;.alisikika Mfugaji akilalamika.

Aidha watumishi waliopo katika taasisi za Umma za NARCO na TALIRI ,West Kilimanjaro nao wamelalamikiwa na wafugaji hao kuwa ni vinara wa kuchukua rushwa hasa Ngombe wa wafugaji wanapokamatwa wakiwa katika maeneo ya Taasisi hizo wakipata Malisho.

Aidha,Wafugaji wa kijiji cha Sanya Station wamemweleza katibu Mkuu kuwa, changamoto kubwa waliyonayo kwa sasa katika kijiji hicho ni pamoja na, uhaba wa maeneo ya Malisho, Mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda wa miaka 30, ambapo mamlaka ya kiwanja cha ndege ya KIA wananataka kuwapora ardhi waliyoridhishwa na Mababu zao ,Eneo halali lenye kubwa wa Hekta Elfu 11, lenye wakazi zaidi ya Elfu ishirini na nne (24,000) katika kata ya Kia.

Changamoto nyingine waliyotaja ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya Majosho ,ukosefu wa visima virefu vya kunyweshea Maji Mifugo na kukosekana kwa Mnada katika Eneo hilo.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha Wafugaji Taifa Bw. Magembe Makoye, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe John Pombe Magufuli kwa Kuwateua Viongozi waandamizi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ukianzia na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Joelson Mpina, Katibu Mkuu Mifugo, Prof.Elisante Ole Gabriel ambao kwa asili wote ni wafugaji.

Makoye amewaasa Wafugaji kufuata kanuni, Taratibu na sheria za nchi ili waendelee
kuheshimika, kwani wafugaji wanajitosheleza kwa kila kitu ndio maana hawajawahi kuomba chakula Serikalini na wanasomesha watoto wao bila tatizo lolote.

Tunaomba Serikali ipime maeneo ya wafugaji ili wamilikishwe kisheria,  Sasahivi kila hifadhi
imeanzisha Mahabusu ya Mifugo, Ngombe wakikamatwa ndani ya hifadhi anapigwa faini ya
Tsh.100,000/= kwa ngombe mmoja. Hii ni rasimu ya sheria ambayo ilikuja kwa wadau tuliikataa, cha kushangaza watu wa Maliasili wanaitumia, hii ni sheria kandamizi ;alisema.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Hai Bw.Lengai Ole Sabaya amepiga Marufuku kwa watendaji wa Vijiji na Vitongoji kupokea fedha yoyote ya Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji. Mhe Sabaya amesema kuwa Migogoro mingi inayotokea ni kwa sababu wananchi wa kifugaji hawashirikishwi  katika ngazi za maamuzi.

Akifanya Majumuisho ya Mkutano huo, Katibu Mkuu Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameishukuru kamati ya Ulinzi na Usalama ya Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa kutatua Migogoro iliyopo kwa Weledi Mkubwa.

Ole Gabriel amesema kuwa Serikali inatambua haki za Wafugaji,katika nchi hii wafugaji ni
wawekezaji, Lakini ni lazima wafugaji wazingatie sheria, kwani wanamchango mkubwa sana katika Uchumi wa Viwanda.

Rais Magufuli anawapenda wafugaji lakini pia yeye mwenyewe ni Mfugaji, ndio maana katika ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 25 yote inaongelea Wafugaji na namna Bora ya kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Prof.Gabriel amesema kuwa changamoto mbalimbali walizozieleza Wafugaji hao zinafanyiwa kazi kwani Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Sikivu.

Pia Katibu Mkuu Mifugo aliwakumbusha wafugaji kuachana na kufuga kwa mazoea, amewambia wakati umefika sasa kubadilika na kuanza kufuga Kisasa na Kibiashara.



Katibu Mkuu Mifugo na Mbunge wa Siha Dr. Mollel wakifurahia jambo mara baada ya Mzee wa jamii ya kimasai kuja kuwasalimia mara baada ya mkutano kumalizika.

Katibu Mkuu akiongea na wafugaji


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni