Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani amesema serikali kupitia wataalam wake sekta ya uvuvi imeanza kufanya tathmini itakayoongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi pamoja na mnyororo wa thamani ili fedha zinazotolewa na serikali zitumike kutoa manufaa chanya katika jamii.
Akizungumza na wanufaika wa vizimba vya kufugia samaki eneo la Kisoko Mkoani Mwanza, wakati wa ziara yake iliyofanyika Desemba 30, 2025 Mhe. Kamani amesema wizara inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa fedha zote zinazopelekwa kwenye miradi zizalishe manufaa chanya kwa wanufaika.
"Lengo la Dkt Samia Suluhu Hassan na maelekezo mahususi aliyotupa ni kwamba sehemu yeyote tunakoweka fedha ni lazima hiyo fedha iwe na manufaa chanya kwa jamii" alisema Mhe. Kamani.
Aidha, Mhe. Kamani alisema Wizara imeanza mazungumzo na sekta binafsi kwa ajili ya kufanya uzalishaji wa vifaranga vya samaki, vyakula vya samaki na teknolojia inayohitajika ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji kwa wanufaika wa mradi huo wa vizimba vya kufugia samaki ambao lengo lake ni kuwainua kiuchumi.
Kuhusu uwezeshwaji wa mikopo kwa wanufaika wa ufugaji samaki kwenye vizimba Mhe. Kamani amesema Wizara imeanza mazungumzo na taasisi zingine za fedha ili kupanua wigo wa kuwakopesha wavuvi mikopo yenye masharti nafuu.
"Kama Wizara tumeanza mazungumzo na kufanya tathmini ya kuzikaribisha taasisi za fedha ili kuwa na wigo mpana na wa uashindani katika kuwakopesha wavuvi wetu , lengo kuwawezesha mikopo yenye masharti nafuu" alisema.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni