Nav bar

Jumatatu, 5 Januari 2026

DKT. BASHIRU AWAPA SOMO WAWEKEZAJI NARCO KAGERA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka wawekezaji waliopo kwenye kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutumia shamba darasa la Mifugo lililopo Wilaya ya Muleba kubadili mfumo wao wa ufugaji.

Balozi Dkt. Bashiru ametoa angalizo hilo mara Januari 02,2026 wakati wa ziara yake ya kutembelea shamba hilo linalomilikiwa na mfugaji binafsi Bw. Shakiru Kyetema ambapo ameonesha kufurahishwa na mpangilio wa shughuli za ufugaji zilizopo shambani hapo hususan kwenye eneo la kilimo, uchakataji na uhifadhi wa malisho ya mifugo.

“Mkoa wa Kagera hapa tuna ranchi sita na zina maeneo makubwa kuliko hata eneo lako hili lakini wafugaji waliopewa hizo ranchi kama wawekezaji hatuoni msukumo wa kuanza mchakato wa kufuga kisasa kwa kuwa na malisho kwa hiyo nadhani baada ya hapa kuna haja kwa njia hiyo hiyo ya shamba darasa kuwaleta wawekezaji wetu” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.

Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa wawekezaji hao hawawezi kufanikisha azma yao bila kuwekeza kwenye malisho yatakayowawezesha kupata mazao bora ya Mifugo kwa upande wa maziwa na nyama.

“Kwa kuwa Jiographia ni ile ile inafanana, jitihada kama hizi hizi unazofanya hapa nadhani ziwe ndo shule kwa hao wawekezaji waje wajifunze unapopata mbegu, namna ulivyoanza, ulivyopata maji na unavyoendelea kutumia malisho haya kuanza kuzalisha ng’ombe wa maziwa” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Balozi Dkt. Bashiru amehitimisha kwa kuelekeza mikataba mipya ya wawekezaji hao iwekwe kipengele cha sharti la kuwekeza kwenye malisho ya mifugo kwa kuwa tayari ipo teknolojia, mbegu za kisasa na mifano ya kilimo cha malisho hayo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Mkurugenzi wa Uendelezaji nyanda za malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza wakichakata nyasi za malisho ya Mifugo kwenye  shamba darasa la Mifugo la Bw. Shakiru Kyetema lililopo Muleba mkoani Kagera Januari 02,2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akimwagilia malisho ya Mifugo mara baada ya kufika kwenye shamba darasa la Mifugo la Bw. Shakiru Kyetema lililopo Muleba mkoani Kagera Januari 02,2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Mmiliki wa shamba darasa la Mifugo lililopo Muleba mkoani Kagera Bw. Shakiru Kyetema, baadhi ya Watendaji wa Wizara na wananchi wengine wakishuhudia namna robota la kutengenezea chakula cha Mifugo aina ya Hei wakati ziara yake shambani hapo Januari 02,2026.

Mtaalam wa Mifugo wa shamba darasa la Ufugaji la Bw. Shakiru Kyetema lililopo Muleba mkoani Kagera Bw. Wilfred Kipkoech (kushoto) akimueleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kulia) namna wanavyotunza ndama wa ng’ombe waliopo shambani hapo wakati wa ziara yake ya ukaguzi na mafunzo shambani hapo Januari 02,2026.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni