◼️Aagiza kusitishwa kwa mipango ya siri ya ugawaji wa vizimba vya biashara
Waziri wa Mifugo na Uvuvi amewaelekeza wasimamizi wa mradi wa soko la kimataifa la dagaa lililopo Chato maarufu kama “Chato Beach” kuhakikisha vizimba vya soko hilo vinawafikia walengwa waliokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwa mradi huo.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo mara baada ya kukagua hatua za ujenzi wa mradi huo Januari 04,2026 ambapo ameelekeza kuanza kutumika kwa mradi huo mara tu utakapokadhibiwa na mkandarasi Februari 28,2026.
“Ni lazima kuwepo na uwazi kuhusu usimamizi wa soko hili na ugawaji wa vizimba vilivyopo hapa na inawezekana mahitaji yakawa makubwa kuliko nafasi zilizopo lakini tunataka mfumo utakaotumika ukiwa wa wazi na haki hata atakayekosa akiri kukosa kwa sababu ya upungufu na sio mizengwe” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amewaelekeza wataalam wa Wizara kukaa pamoja na wale wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato ili kupanga utaratibu wa kumpata mwendeshaji wa soko hilo na mtambo wa kuhifadhi ubora wa dagaa kupitia ukaushaji.
“Ni bora mtambo wa kukausha dagaa ukamilike mengine yasubiri kwa sababu taarifa za wataalam zinatueleza kwamba asilimia 30 ya dagaa wanaovunwa wanaharibika kwa sababu hatuna teknolojia ya ukaushaji na tukikausha kwa teknolojia duni ubora wa dagaa zetu unashuka” Amehitimisha Balozi Dkt. Bashiru.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni