Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesikitishwa na hali ya utekelezaji wa shughuli za mnada wa kimataifa wa Mifugo wa Buzirayombo uliopo Chato mkoani Geita.
Balozi Dkt. Bashiru ameonesha masikitiko hayo mara baada ya kufika na kukagua hali ya mnada huo Januari 04,2026 ambapo mbali na kutoridhishwa na hali ya mazingira ya mnada huo ameshangazwa kwa kutotumia mizani wakati wa uuzaji wa mifugo.
“Nataka ndani ya wiki mbili kuanzia leo mnada huu uwe na maji kwa sababu tenki lipo, miundombinu ipo imara, chanzo cha maji yanapotoka kipo lakini pia tuna akiba ya tenki la chini halafu hakuna maji kwenye mradi mkubwa wa namna hii wa Bil. 4, kwanza hatukustahili kuanza kuutumia bila mfumo wa maji kukamilika” Amesisitiza Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha balozi Dkt. Bashiru ameshangazwa na suala la wafanyabishara wa mnada huo kukataa kutumia mizani wakati wakinunua mifugo mnadani hapo ambapo amesisitiza kuwa kitendo hicho kinaitia hasara Serikali ambayo imetenga fedha za kujenga mizani hiyo.
“Huwezi kuwekeza pesa kubwa kiasi hiki na mzani halafu mlitaka mimi niangalie sinema ya kitu ambacho hakitumiki na tar 25 nilipita nikielekea Kagera nikafanya ziara mwenyewe na nilizungumza na wananchi wakaniambia humu hamjawahi kuingiza mifugo” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Balozi Dkt. Bashiru amemwelekeza Mhandisi wa Wizara Bw. George Kwandu kumuwasilishia taarifa ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa mnada huo kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi inayotarajiwa kujumuisha miundombinu iliyosalia katika mnada huo.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni