Na. Martha Mbena, Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa kutekeleza mikakati inayolenga kuboresha sekta ya lishe kwa kuifanya kuwa na mifumo endelevu nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede wakati akifungua kikao cha kujadili mradi wa Initiative on Climate Action and Nutrition (I-CAN) kilichofanyika leo Oktoba 16, 2025 katika Hoteli ya Rafiki Jijini Dodoma.
Dkt. Mhede amesema serikali inafanya kazi na wadau na mashirika mbalimbali kwa kufanya majadiliano ya jinsi ya kuoanisha masuala ya kisera katika mabadiliko ya tabianchi na lishe bora.
"Yaliyojadiliwa kwenye kikao cha leo yawe chachu ya kuifanya sekta hii ya lishe isogee mbele zaidi lakini mkakati wa mapitio ya sera kuhusu masuala ya lishe ni jambo la muhimu ", amesema Dkt. Mhede.
Amesema wananchi wanategemea kupata afua za serikali zinazohimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki kwa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Naye, Mkuu wa miradi kutoka Shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) Dkt. Winfrida Mayilla amesema kikao hicho kimelenga kuyatambua masuala ya hali ya hewa na uhusiano wake kwenye lishe na kwa kuzingatia sera za nchi.
"Tuko hapa na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba sera zetu za Nchi hasahasa sera ya chakula na lishe inaingiza mikakati ya kuboresha mabadiliko haya ya tabianchi na tuje na mbinu mbalimbali ili tukifanya kazi kwa pamoja ilenge kuboresha afya na lishe za watanzania" amesema Dkt. Mayilla.
Kikao cha mradi wa Initiative on Climate Action and Nutrition (I-CAN) kimejadili mabadiliko ya tabianchi, lishe bora pamoja na sera za kitaifa na uhusiano wake katika kuwekeza kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi unaostahimili mabadiliko ya hali ya hewa.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni