Nav bar

Jumatatu, 27 Oktoba 2025

MEENA ATAKA USHIRIKIANO, TAASISI SITA ZA MIFUGO KUWA JENGO MOJA

Na. Edward Kondela

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amezitaka taasisi sita kutoka sekta ya mifugo zinazojenga ofisi zake katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, kusimamia ujenzi huo kwa ushirikiano ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyotarajiwa.

Bi. Meena amebainisha hayo leo (21.10.2025) kwenye tukio la utiaji sahihi wa mkataba wa ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya taasisi hizo, zilizo chini ya wizara na kukabidhi eneo kwa mkandarasi wa ujenzi wa jengo hilo, ambapo amesema kukamilika kwa ujenzi kutasaidia kuondokana na tatizo la ukosefu wa ofisi bora kwa watumishi.

Akizungumzia juu ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambazo zitakuwa kwenye jengo moja, amesema anatambua TALIRI ndiyo imeingia makubaliano ya kimkataba lakini taasisi zingine tano zisijiweke kando bali zishiriki katika kusimamia ujenzi huo.

Aidha, amemtaka mkandarasi wa ujenzi Kampuni ya CJIETC kutoka China na mkandarasi mshauri wa ujenzi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufanya kazi kwa bidii na umahiri mkubwa ili ujenzi ukamilike kwa wakati na viwango vya juu kama ilivyoonyeshwa kwenye mkataba wa ujenzi wa miezi 24 pamoja na mwaka mmoja wa uangalizi.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wengine wa taasisi zitakazotumia jengo hilo baada ya kukamilika kwake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba, amesema wametumia mfumo ambao ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inaratibu ujenzi wa majengo ya serikali jijini Dodoma, imeufurahia kwa taasisi hizo sita kutumia jengo moja katika eneo la ekari 10.

Pia, amesema ofisi ya Waziri Mkuu imesema itashawishi taasisi zingine zilizopo kwenye wizara mbalimbali kutumia mfumo huo wa kuwa na jengo moja, hivyo kurahisisha huduma kwa wananchi.

Naye Mkadiriaji Majenzi kutoka Kampuni ya CJIETC kutoka China Mhandisi Wencleaus Kiziba amesema watahakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa wakati na kulingana na bajeti ya fedha iliyotengwa pamoja na kuzingatia ubora.

Ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya TALIRI, TDB, LITA, TVLA, TMB na NARCO unatarajia kutumia takriban shilingi bilioni 54 zote kwa pamoja, ambapo mkandarasi atatekeleza kwa shilingi bilioni 49, TBA ambaye ni mshauri elekezi shilingi bilioni 4.5.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (katikati), akiwa na viongozi wa taasisi za mifugo zilizo chini ya wizara hiyo wakati akikata utepe wa ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya TALIRI, TDB, LITA, TVLA, TMB na NARCO katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma. (21.10.2025)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena, akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba na mwakilishi wa Kampuni ya CJIETC kutoka China ambayo itajenga jengo la ofisi za makao makuu ya TALIRI, TDB, LITA, TVLA, TMB na NARCO katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma na kushuhudia kazi ya kusafisha eneo hili ikiwa imeshaanza. (21.10.2025)

Muonekano wa picha ya jengo litakalojengwa katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma kwa ajili ya ofisi za makao makuu ya taasisi sita zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambazo ni TALIRI, TDB, LITA, TVLA, TMB na NARCO ambapo ujenzi wake utagharimu takriban shilingi bilioni 54 hadi kukamilika kwake. (21.10.2025)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (aliyekaa kulia), akishuhudia utiaji sahihi kati ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Kampuni ya CJIETC kutoka China ambayo itajenga jengo la ofisi za makao makuu ya TALIRI, TDB, LITA, TVLA, TMB na NARCO katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma. (21.10.2025)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba (katikati) na mwakilishi wa Kampuni ya CJIETC kutoka China ambayo itajenga jengo la ofisi za makao makuu ya TALIRI, TDB, LITA, TVLA, TMB na NARCO katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, baada ya kutia sahihi mkataba wa ujenzi wa jengo hilo. (21.10.2025)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni