Nav bar

Jumanne, 8 Julai 2025

MHE: MNYETI: “MASHAMBA YA SERIKALI YAACHWE KWA MANUFAA YA TAIFA”

Na. Edward Kondela – WMUV, Mwanza

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali lazima yaachwe yafanye shughuli za serikali kwa ajili ya manufaa ya taifa zima.

Naibu Waziri Mnyeti amebainisha hayo (07.07.2025) katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, alipofanya ziara katika shamba hilo kufuatilia utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, ambapo amesema mashamba hayo lazima yaendelezwe kwa kuwa ni rasilimali ya taifa.

Mhe. Mnyeti amesema kuwa mifugo iliyopo katika mashamba ya serikali ni kama mbegu ambazo lazima kuzitunza ili kutoharibu mbegu za asili za mifugo.

“Mashamba ya serikali ni rasilimali za watanzania wote lazima kulinda kwa pamoja, hizi ng’ombe ni kama mbegu tukiziharibu hizi mbegu ni kwamba tunaharibu kabisa ng’ombe zetu za asili.”

Naibu Waziri Mnyeti amebainisha hayo baada ya taarifa ya kuwepo kwa uvamizi wa mifugo kuingizwa katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki kwa ajili ya malisho.

“Ng’ombe 20,000 waliovamia Shamba la Mabuki siyo wa wafugaji wa Misungwi isipokuwa wafugaji wa Misungwi wamekuwa siyo waaminifu kwa kukumbatia makundi ya ng’ombe kutoka nje ya Misungwi halafu wanajifanya ni ng’ombe wao.” amebainisha Mhe. Mnyeti

Ameongeza kuwa hayuko tayari kuwatetea wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali kwa kuwa hata yeye ni mfugaji lakini anaheshimu maeneo yaliyotengwa na serikali, yakiwemo mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali na kwamba hayuko tayari kupeleka mifugo yake kwenye mashamba hayo bila kufuata utaratibu wa serikali.

Kuhusu utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki, Mhe. Mnyeti amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza mifugo yote yenye sifa ya kuwekewa hereni lazima itambulike ili kuwezesha pia kufahamu idadi ya mifugo iliyopo nchini.

Aidha, amewaarifu wafugaji kuwa zoezi la uchanjaji wa mifugo linaenda sambamba na uwekaji wa hereni bure, ambapo hereni hizo pia zitasaidia katika kudhibiti wizi wa mifugo nchini.

Naye Kaimu Meneja wa Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki Bi. Lini Mwala amesema katika shamba hilo wanatarajia kuchanja ng’ombe zaidi ya 3,000, mbuzi na kondoo zaidi ya 1,500 katika kudhibiti magonjwa ya mifugo.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa Wilaya ya Misungwi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji katika wilaya hiyo Bw. Bukula Muhoja amesema kama chama kuanzia ngazi ya taifa walishaanza uhamasishaji kwa kutoa elimu kwa wafugaji ili wachanje mifugo yao.

Ameongeza kuwa kwa Wilaya ya Misungwi wamesimamia kila kata na kijiji kuhakikisha wanazungumza na wafugaji ili kuchanja mifugo yao na kwamba wamepokea kampeni hiyo kwa mikono miwili.

Kampeni hii serikali imetoa ruzuku ya asilimia 100 kwa kuku ambapo watachanjwa bure huku ng’ombe, mbuzi na kondoo ikitoa ruzuku ya asilimia 50.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akikagua hereni ya kieletroniki iliyowekwa kwenye sikio la ng'ombe wakati wa ziara ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki, lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. (07.07.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akifuatilia namna taarifa muhimu za hereni za kieletroniki zinavyojazwa kwenye kishikwambi, wakati wa ziara ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki, lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. (07.07.2025

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi (udhibiti magonjwa yaenezwayo na wadudu), Dkt. Christopher Sikombe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza Mhe. Johari Samizi, juu ya taarifa muhimu zilizopo kwenye hereni za kieletroniki kwa ajili ya mifugo wakati wa ziara ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki. (07.07.2025)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni