Na. Omary Mtamike
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewashukuru wafugaji nchini kwa utayari wao kwenye utekelezaji wa mpango wa kuboresha sekta ya Mifugo nchini hususan upande wa kampeni ya Chanjo na Utambuzi iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Dkt. Kijaji ametoa shukrani hizo Julai 07, 2025 kwenye ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni hiyo Wilaya ya Urambo mkoani Tabora ambapo ameonesha kufurahishwa na ushirikiano ambao wafugaji wameutoa kwa Serikali kwenye maeneo yote aliyopita.
“Serikali inawahakikishia wafugaji kuwa daima itaendelea kuboresha mazingira yenu ya ufugaji na ndio maana mmeona wenyewe jinsi Rais Samia alivyoamua kugharamia utambuzi wa Mifugo yote nchini zoezi ambalo awali lililalamikiwa kutokana na gharama zilizokuwa zinatozwa za shilingi 700 kwa ng’ombe mmoja” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji
Akigusia changamoto ya wafugaji wengi kukosa maeneo yao ya malisho, Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa Rais Samia ametoa maelekezo kwa Wizara yake, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kuainisha mipango ya matumizi bora ya ardhi ili wafugaji waoneshwe maeneo yao.
“Kwa hiyo kwa unyenyekevu nikuombe Mhe. Mkuu wa mkoa utusaidie kufahamu maeneo hayo na sisi Wizara tutahakikisha yanapata hati na kutambuliwa kama maeneo ya Wafugaji” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.
Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mkoa wa Morogoro Julai 10, 2025.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni