Na. Stanley Brayton
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua zoezi la Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Kitaifa, Juni16, 2025 Mjini Bariadi, mkoani Simiyu.
hayo yamefahamika wakati Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiongea na Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo Juni 11, 2025, ambapo amesema uzinduzi huo wa Kampeni ya chanjo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuboresha afya ya mifugo hapa nchini ambayo inakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 39.2, mbuzi milioni 28.6, kondoo milioni 9.7, kuku milioni 108.2 na nguruwe milioni 4.1.
“Pamoja na idadi hii ya mifugo bado mchango wa sekta hii kwenye pato la taifa mpaka sasa ni 6.2%. Mchango huu ni mdogo ukilinganisha na idadi ya mifugo tuliyo nayo, na moja ya sababu ya mchango wa sekta ya mifugo kuwa mdogo kwenye pato la Taifa ni uwepo wa magonjwa mbalimbali ya wanyama ambayo huathiri uzalishaji wa mifugo kwa kusababisha vifo vya mifugo na hata kukosekana kwa ithibati ya kuuza mifugo na mazao yake katika masoko ya kimataifa.” ameseama Mhe. Dkt. Kijaji
Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji amesema kwa kutambua umuhimu wa Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo hususan katika biashara za wanyama na mazao yake katika masoko ya kimataifa, zoezi hili la la uchanjaji litaenda sambamba na Utambuzi na Usajili wa mifugo kwa uvishaji wa hereni za kieletroniki kwa Wanyama wote watakaochanjwa.
Vilevile, Mhe. Dkt. Kijaji amesema Kampeni hiyo ya chanjo itatekelezwa na wataalamu wa Serikali katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa, na pia itawashirikisha vijana waliohitimu kwenye vyuo vya Mafunzo ya Mifugo ambao bado hawajapata ajira ya Serikali, kwa kutoa ajira za muda mfupi kwa vijana wapatao 3,540 ambao ni wataalam wa Afya ya Wanyama walioko nje ya ajira rasmi.
Halikadhalika, Mhe. Dkt. Kijaji amewataka Wafugaji kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa kupeleka mifugo yao kwenye vituo vya chanjo kama ratiba za uchanjanji zitakavyoelekeza katika maeneo yao,na watumie fursa hiyo vizuri kwa ustawi wa mifugo yao.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni