Nav bar

Ijumaa, 2 Mei 2025

SERIKALI YAKABIDHI GARI LA UBARIDI KWA CHAMA CHA USHIRIKA WA UVUVI BUKASIGA

Na Hamisi Hussein, WMUV - Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhi gari la ubaridi kwa ajili ya kusafirishia mazao ya uvuvi kwa Chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA Ltd kilichopo  Wilaya ya Ukerewe Jijini Mwanza  ikiwa ni utekelezaji wa Mpango  wa kuboresha usimamizi wa uvuvi, ukuzaji wa viumbe maji, uchumi wa buluu na biashara katika ukanda wa SADC (PROFISHBLUE).

Akikabidhi gari hilo kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, leo Aprili 30, 2025 katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amesema serikali inaendelea kuwawezesha wananchi wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi ikiwemo chama cha  Ushirika wa uvuvi BUKASIGA 

”Serikali imetumia rasilimali zake kuhakikisha BUKASIGA Ltd inasimama, ndio ilisaidiwa na serikali wakati wa kuingia kwenye mchakato shindani wa mradi wa Profishblue ambao unatumia fedha za serikali kupitia  Benki ya Maendeleo ya Africa (ADB) mradi unaolenga kuongeza ubora wa mazao na kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi, kwahiyo gari hili likafanye kazi iliyokusudiwa na likasafirishe Samaki tu”  amesema Dkt. Mhede.

Aidha Dkt. Mhede amemwagiza Kaimu  Mkurugenzi wa Uvuvi Dkt. Baraka Sekadende  kukisaidia Chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA  kufanya usajili gari hilo  pamoja na kuliweka chapa ’branding’ zitakazoonesha usafirishaji wa mazao ya Samaki ili lisitumike kwa matumizi mengine.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi  wa Uvuvi Dkt. Baraka Sekadende akizungumza  kwenye hafla hiyo amesema kuanzia mwaka 2019 wizara imefanikiwa kuanzisha vyama vinne vya ushirika wa uvuvi ikiwemo  cha BUKASIGA Ltd ambacho ndicho kimekabidhiwa  gari hilo litakalopunguza upotevu wa mazao ya uvuvi .

Naye Mwakilishi wa sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza ambaye ni Mrajisi wa Ushirika mkoani humo Bi. Hilda Boniface ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuvisaidia vyama vya ushirika kukua kupitia sekta ya uvuvi na kutoa wito kwa vyama vyote vya ushirika kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali, huku Mwenyekiti wa chama cha Ushirika  BUKASIGA Ltd Bw. Erasto Majura akiishukuru serikali  na kuahidi kulisimamia gari hilo liweze kuwanufaisha wanachama na jamii kwa ujumla.

Gari ya ubaridi iliyokabidhiwa kwa chama cha ushirika wa Uvuvi cha Bukasiga ina thamani ya dola za kimarekani 87,230.99, pia gali hilo linakadiriwa  kuhifadhi  samaki kwa muda wa mwaka mmoja ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa PROFISHBLUE unaotekelezwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede ( Kushoto) kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimkabidhi  Kadi ya Gari la Ubaridi litakalotumika kusafirishia mazao ya Uvuvi ya chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA LTD Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Erasto Majura( Kulia)  wakati wa hafla ya makabidhiano ya Gari la Ubaridi kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma, Aprili 30, 2025.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede ( Wa tatu, kulia) kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi akizungumza na Wanachama wa Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA LTD  pamoja na baadhi ya Wataalamu kutoka wizarani wakati wa hafla ya makabidhiano ya Gari la Ubaridi kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma, Aprili 30, 2025.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede ( Kushoto) kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akikagua Gari hilo la Ubaridi litakalotumika kusafirishia mazao ya Uvuvi kabla ya kukabidhi kwa chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA Ltd, hafla iliyofanyika kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma, Aprili 30, 2025.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede ( wa kwanza, kulia) kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akitoa Maelekezo kwa Wataalamu wa Wizara juu ya usajili wa Gari la Ubaridi litakalotumika kusafirishia mazao ya Uvuvi ya chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA LTD wakati wa hafla ya makabidhiano ya Gari la Ubaridi kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma, Aprili 30, 2025.

Gari la Ubaridi litakalotumika kusafirishia mazao ya Uvuvi  ya Chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA LTD limekabidhiwa na Naibu Katibu Mkuu( Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa PROFISHBLUE hafla ya makabidhiano imefanyika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma, Aprili 30, 2025.








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni