Nav bar

Alhamisi, 20 Julai 2023

SERIKALI YAWEKA NGUVU KATIKA UTAFITI WA RASILIMALI ZA BAHARI NCHINI ILI KUWA NA UVUVI ENDELEVU

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Serikali ya Norway imepokea meli ya utafiti ya Dr. Fridtjof Nansen ambayo inafanya utafiti wa ikolojia ya Bahari na rasilimali za uvuvi zinazopatikana katika Bahari ya Hindi na kusaidia kuimarisha usimamizi wa Rasilimali za Bahari.


Akiongea, katika hafla ya kuipokea rasmi meli hiyo katika Bandari ya Dar es salaam leo 11 Julai 2023, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame, amesema utafiti huo unafanyika Tanzania Bara na visiwani (zanzibar) na utatoa taswira ya aina za samaki wanaopatikana  baharini kwa ajili ya kuweka mipango madhubuti ya usimamizi. Utafiti huo, umeanza kufanyika 28 Juni 2023 na utakamilika 28 Julai 2023. 


"Tumekuwa tukifanya uvuvi bila kujua ni aina gani ya samaki na viumbe wengine wa Bahari tulionao, kwa hiyo tutakapokuwa na takwimu sahihi za rasilimali za samaki waliomo baharini tutaweka mkakati wa kudhibiti mazao ya baharini hasa aina za samaki ambao wamekaribia kutoweka." amesema Makame.


Mhe. Makame amesema ni mara ya tatu utafiti kama huu unafanyika katika eneo la bahari nchini Tanzania, kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 1982, mara ya pili ukafanyika mwaka 2018 na sasa unafanywa mara ya tatu na meli ya Dr Fridtjof Nansen.


Amesema baada ya kukamilika kwa utafiti huo Julai 25 mwaka huu Serikali itafahamu aina za samaki waliomo Baharini na tumeambiwa kuna aina mpya za samaki ambao hawajawahi kuonekana lakini kupitia utafiti huu, aina hizo zitawekwa katika rekodi ya dunia.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimerei amesema utafiti unaofanyika ni muhimu katika kupata uhalisia wa kiasi cha samaki waliopo katika maji Baharini. 


"Hadi sasa kiasi cha samaki kinachokadiliwa kuwemo katika maji ya ni tani 100,000 utafiti huu ulifanyika 1982, takwimu za 2018 hazitumiki kwasababu hazikuwa sawa,


 "Tunaamini utafiti unaokwenda kufanyika sasa utatoa majibu sahihi na tutayasilisha Wizarani kwa ajili ya matumizi ya Wizara ikiwemo utungaji wa  Sera ,"amesema Kimerei.


Dkt. Kimerei amesema katika meli hiyo wapo watafiti 25 wakiwamo 13 kutoka Tanzania.


Kwa upande wake Mwakilishi mkazi wa Shirika la FAO Tanzania Dkt. Nyabenyi Tito Tipo amesema, wanatambua umuhimu wa kusaidia ukuaji wa sekta ya uvuvi Tanzania hivyo wataendelea kuishika mkono Serikali na kushirikiana na wadau wengine kuendeleza rasilimali za bahari.


Amesema takwimu zitakazopatikana kwenye utafiti huo zitakuwa hazina ya Tanzania. Meli hiyo ya utafiti imejumuisha watafiti kutoka Kenya, Msumbiji Afrika kusini, Australia na Norway


Tanzania inakusudia kuwa na takwimu za rasilimali zilizopo baharini pamoja na kuweka mkakati wa uvuvi kwa lengo la kudhibiti shughuli za uvuvi na ulinzi wa rasilimali za samaki walio hatarini  kutoweka vilivyo hatarini kutoweka. hii ni baada ya kuruhusu Serikali ya Norway pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula(FAO) kuanza utafiti wa rasilimali zilizopo baharini kwa Tanzania bara na visiwani

Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  Mhe. Suleiman Makame akihutubia kwenye hafla ya kupokea meli iliyokuja kwa ajili ya kufanyia Utafiti wa aina mbalimbali ya viumbe wanaopatikana Bahari ya Hindi  ya (Dr. Fridtjof Nansen) katika bandari ya Dar es salaama leo 11 Jully 2023.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  Mhe. Suleiman Makame akimsikiliza Captain Tommy Steffensen anayeisimamia meli ya Utafiti ya DR. FRIDTJOF NANSEN, akimuelezea na kumuonyesha sehemu ambayo Captain wa meli anafanya shughuli ya kuiendesha meli hiyo.kwa kutumia vifaa vya kiteknolojia ya kisasa, wakati wa hafla ya kuipokea Meli hiyo iliyofanyika katika Bandari ya Dar es salaam (Port Call Event), 11 Julai 2023.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame (watatu kulia) akimsikiliza mhudumu wa kwenye meli ya DR. FRIDTJOF NANSEN ambaye yupo kwenye eneo la Maabara ya samaki (Fish Lab) akimuelezea na kumuonyesha aina mbalimbali za samaki ambazo wanafanyia utafiti kwenye meli hiyo iliyofika nchini kwa ajili ya kufanya utafiti wa Viumbe wa baharini, wakati wa hafla ya kuipokea meli ya utafiti katika Bandari ya Dar es salaam, 11 Julai 2023.

Muonekano wa meli kubwa ya kimataifa ya Dr. Fridtjof Nansen kwa ajili ya kufanya  Utafiti ambao utasaidia Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Nchini, imeanza utafiti tarehe 28 Juni 2023 na inatarajia kumaliza Utafiti huo 28 Julai 2023.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  Mhe. Suleiman Makame (waliokaa, katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakuu wa Idara, wakuu wa Taasisi na Wenyeviti kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya Uvuvi,  mara baada ya hafla ya kupokea meli ya Utafiti katika Bandari ya Dar es salaam,  leo tarehe 11 Julai 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni