Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

WAFUGAJI WATAKIWA KUANZA KUPANDA MALISHO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amesema ili kuondokana na migogoro kati ya wafugaji na wakulima pamoja na  maeneo ya hifadhi, wanatakiwa   kuanza kuzalisha  mazao ya ziada kwa ajili ya mifugo yao.


Mhe. Ndaki aliyasema hayo Aprili 21,2022 jijini Dodoma wakati alipokutana na chama Cha wafugaji Tanzania CCWT ambapo alisema wafugaji wawe wabunifu kwa kuzalisha malisho kwa mifugo wakati wa ukame ili kuokoa upotevu wa mifugo wakati wa kiangazi.


Alisema, Serikali imelifanyia upembuzi yakinifu suala la malisho kwa kuandaa muongozo wa malisho, na muongozo huo umefafanua ni kwa namna gani maeneo ya malisho yatatengwa na kulindwa kwa ajili ya mifugo. 


Aliongeza kuwa pamoja na kuwa na miongozo bado tuna matatizo ya malisho na maji. 


"Ni muhimu kuchukua tahadhari kwenye maeneo yetu ya malisho kwa kufuata muongozo kutoka kwa wataalamu wetu" alisema Ndaki.


Aidha, Mhe. Ndaki alisema, kwenye maji Wizara imejitaidi kuchimba malambo kadhaa,  na Serikali imenunua vifaa vya kuchimba malambo.


"Niwaombe wafugaji kama ikihitajika kuchangia gharama za uchimbaji tuwe tayari  kuchangia gharama hizo na hao watakaowekwa kwenye kuchangisha gharama hizo wawe waaminifu kukusanya pesa hizo wasiwe wabadhilifu" alisema Ndaki. 


Naye Spika wa bunge mstaafu, Bi. Anna Makinda aliwapongeza  wafugaji kwa kusema matatizo yao kwa ukweli kwa kuwa ni njia nzuri ya kutatua changamoto zao na inasaidia Serikali kujua ni wapi hawajaweka nguvu ya kutosha.


Kwa upande wake mwenyekiti wa Cha wafugaji Tanzania Jeremia Wambura, alisema chama cha wafugaji Tanzania kimejipanga kufuga kwa tija ikiwa ni pamoja na kukuza soko la nyama nje ya nchi.


Wambura alisema, katika kuhakikisha zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu wafugaji wamehimizwa kutoa taarifa za kweli wakati wa kuhesabiwa huku mjumbe wa bodi ya chama Cha wafugaji Tanzania akaomba ushirikiano baina ya wafugaji na serikali.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni