Nav bar

Jumatano, 29 Septemba 2021

ULEGA AINGILIA KATI MGOGORO SHAMBA LA SERIKALI NANGARAMO NA WANANCHI


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu kuweka utaratibu mzuri wa kugawa kwa muda sehemu ya shamba la kuendeleza Mifugo la Nangaramo na kuwapatia wananchi wanaoishi karibu na shamba hilo ili waweze kufanya shughuli zao za kilimo.

Ulega alitoa maelekezo hayo Septemba 24, 2021 kufuatia malalamiko aliyoyapata kutoka kwa wananchi wanaoishi karibu na shamba hilo kukosa maeneo ya kulima wakidai kuwa mipaka ya shamba hilo imewekwa ndani ya maeneo yao ya asili ya kilimo.

Akiwa katika shamba hilo lililopo Wilayani Nanyumbu, Mkoani Mtwara, Naibu Waziri Ulega alipata fursa ya kusikiliza kero za wananchi hao ambao wengi wao waliiomba Serikali kuwapatia sehemu ya eneo la shamba hilo ili waweze kulima zao la mpunga.

Baada ya kusikiliza malalamiko ya Wakulima hao ambao walisema maeneo yao yamechukuliwa na shamba hilo, Ulega alimuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kupitia upya maeneo ya mipaka ya shamba hilo ili waone ni sehemu gani katika shamba hilo wanaweza kuligawa kwa muda kwa Wakulima hao.

 

"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya asipewe mtu kipande cha kulima bila kuwa na karatasi ya makubaliano itakayothibisha muda wa kulima katika eneo hilo, maana bila kufanya hivyo kuna wachache wanaweza kugeuka huko mbele wakauza maeneo hayo wakati yeye alipewa kwa muda tu," alisema Ulega

Naibu Waziri Ulega aliendelea kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Samia Suluhu Hassan inatumia maarifa makubwa sana katika kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo na hivyo aliwataka wananchi hao kuendelea kulitunza shamba hilo na wasigombane na Uongozi wa shamba hilo, wakae kwa amani na upendo ili waweze kufanya shughuli zao vizuri.

"Shamba hili ni lenu Watanzania wote litunzeni, muwe na wivu na shamba hili, msimuone mtu analifanyia ubaya na nyie mkafurahia, hapana, msifanye hivyo litunzeni ni mali yenu,"alisisitiza Ulega

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa maelekezo yake wameyapokea na watayafanyia kazi.

"Mheshimiwa Naibu Waziri tunakuahidi tutasimamia maelekezo yako na tunaamini wakati wa mvua ukifika Wakulima hawa wakianza kulima katika maeneo tutakayo wagawia lugha itakuwa tofauti hapa," alisema Chaurembo

Awali, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, Yahya Mhata alisema kuwa ni muhimu Serikali kuangalia upya mipaka ya shamba hilo ambalo sehemu kubwa kumekuwa pori bila kutumika, huku akimuomba Naibu Waziri Ulega kuona uwezekano wa kutoa baadhi ya eneo na kuwagawia Wakulima ili waweze kufanya shughuli zao za Kilimo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alitoa maelekezo ya kuboresha shamba la kuendeleza mifugo la Nangaramo kwa Meneja wa Shamba hilo (kulia kwake- aliyevaa Shari jeupe) alipotembelea katika shamba hilo Septemba 24, 2021. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo

Sehemu ya Wananchi wanaoishi karibu na shamba la kuendeleza Mifugo la Nangaramo lililopo Wilayani Nanyumbu, Mkoani Mtwara wakiwa wanamsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (hayupo pichani) alipotembelea Shamba hilo Septemba 24, 2021. 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni