Nav bar

Jumatano, 29 Septemba 2021

SERIKALI YADHAMIRIA KUBORESHA BIASHARA YA MIFUGO NCHINI.

 


Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo, ikiwemo ujenzi wa mnada wa upili wa nyamatala ili kuendelea kuchochea uchumi wa taifa.

Hayo yalisemwa   na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Amosy Zephania, wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mifugo wa mnada wa upili Nyamatala uliopo Wilayani Misungwi mkoani Mwanza Septemba 27,2021.

Alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa mifugo kukutana na wenye viwanda, wazungumze na kukubaliana bei ili kuwezesha upatikanaji wa mifugo yenye ubora ambao unahitajika kwenye viwanda na wafanyabiashara hao kupata soko zaidi.

"Lengo ni kuendelea kuona mifugo inapata thamani, ambapo watu wa viwandani wanadai kuwa mifugo wanayopelekewa haina ubora wanao wanaouhitaji." Alisema

Aliongeza kuwa wanaposema biashara, wanaanzia sokoni, Wizara pamoja na serikali kwa ujumla mpaka sasa ina viwanda vitano vikubwa vinavyotegemea malighafi za mifugo ikiwemo kiwanda cha Chobo Misungwi na Tan Choice.

"Sisi tumekuja kutoa rai kwenu, wenye viwanda waje wazungumze na nyinyi, wawaeleze wanataka mifugo ya aina gani, mifugo inenepeshwe kwa kiwango gani na watatoa bei gani, Alisema Bw. Zephania.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mifugo mnada wa upili Nyamatala Bw. Emmanuel Mgelwa, aliipongeza serikali kuwatimizia mahitaji waliokuwa wanayataka katika mnada huo ila changamoto ni suala la ulinzi.

Naye Tabu Shindika, aliiomba serikali kuleta mnada wa mbuzi katika eneo hilo ili mtu akitaka ng'ombe, mbuzi na kondoo wapate hapo kwenye mnada wa Nyamatala.


Kaimu katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Amosy Zephania akiongea na wafugaji pamoja na wafanyabiashara wa Mifugo wa mnada wa Upili nyamatala wakati wa ziara yake Mkoani Mwanza. Lengo ni kujua changamoto zinazowakabili katika biashara yao na kujadili njia Bora za kuweza kutatua changamoto hizo kwenye mnada Huo Mkoani Mwanza. Septemba 27,2021



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni