Nav bar

Ijumaa, 13 Agosti 2021

WAKAGUZI WATAKIWA KISIMAMIA UBORA WA VYAKULA VYA MIFUGO

Serikali imewataka wakaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo kuhakikisha mifugo inapatiwa vyakula vyenye ubora na stahiki ili kuondokana na madhara ya sumukuvu yanayoweza kuwaathiri walaji wa nyama, mayai, maziwa na bidhaa nyingine za mazao ya mifugo.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bw. Peter Nyakigera wakati akifungua mafunzo ya wakaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo yaliyofanyika leo Agosti 12, 2021 katika ukumbi wa siasa ni kilimo Mkoani Iringa.

Nyakigera alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa wakaguzi walio kwenye mamlaka za serikali za mitaa kwa vile yatasaidia kutatua changamoto ya ubora na viwango hafifu vya vyakula vya mifugo vinavyotumiwa na wafugaji walio wengi ambapo hata vifo vya baadhi ya mifugo vimesabishwa na kutumia baadhi ya rasilimali za vyakula vyenye sumukuvu.

“Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo Afrika ikiwa na ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, kondoo milioni 5.65, kuku milioni 83.28 ambapo kwa mwaka 2019/2020 zilizalishwa hadi lita bilioni 3.01 za maziwa, tani 701,679 za nyama na mayai bilioni 4.05 hivyo uzalisaji wa mazao haya kwa kiasi kikubwa unategemea upatikanaji wa uhakika wa rasilimali za vyakula vya mifugo vyenye ubora na viwango stahiki” alisema Bw. Nyakigera.

Nyakigera alisema kuwa wakaguzi hao wanawajibu mkubwa wa kulinda afya za walaji na mifugo yenyewe kwa kusimamia sheria na kanuni ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa wadau kwenye mnyororo wa thamani kwenye tasnia ya vyakula vya mifugo.

Aliongeza  kuwa elimu ya ufugaji wenye tija inayoendelea kutolewa imeongeza hamasa kwa wafugaji  hivyo ni  muhimu kupatikana kwa vyakula vyenye ubora na viwango  hususani kwa ng’ombe na kuku.

“Kuwepo kwa vyakula vyenye ubora kutapuguza malalamiko ya ukuaji hafifu uliobainika kwa kuwa wafugaji hutumia takribani asilimia 60 ya gharama zote za uzalishaji kwenye vyakula, hivyo uzalishaji wenye tija hutegemea sana uwepo wa viini lishe vyote muhimu kwenye vyakula hivyo” amemalizia Nyakigera.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Rogers Shengoto alisema mafunzo hayo ni moja ya utekelezaji wa majukumu yaliyopangwa na Idara hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha changamoto za ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa na vinavyotumiwa na wafugaji nchini vinakuwa vimezingatia kanuni bora, sheria na taratibu zote ambazo zinatakiwa.

"Tunataka kuhakikisha changamoto za ubora kwa malalamiko ya ukuaji wa wanyama na uzalishaji hafifu unapungua kwa wazalishaji wa Mifugo. Amesema Bw. Shengoto.

Naye Mkaguzi wa maeneo ya malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo kutoka Mkoa wa Babati, Bw. Mayanzi Bubinza ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa wafugaji na wataalam nchini.


Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Rogers Shengoto (wa pili kutoka kulia) akimueleza machache Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji Mkoa wa Iringa Bw. Peter Nyakigera (kushoto) kabla ya ufunguzi wa mafunzo kwa wakaguzi wa maeneo ya malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo nje ya ukumbi wa siasa ni kilimo halmashauri ya wilaya ya Iringa Mkoani  Iringa  Agust 12, 2021.

Kaimu Mkurugenzi wa  Rasilimali za vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Bw. Rogers Shengoto,  akimkaribisha mgeni rasmi (hayupo pichani) Ili kuweza kufungua mafunzo ya wakaguzi wa maeneo ya malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo kwenye ukumbi wa siasa ni Kilimo halmashauri ya wilaya ya Iringa Mkoani Iringa  Agosti 12, 2021.

Baadhi ya wataalam wakitoa wafunzo kwa wakaguzi wa maeneo ya malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo kwenye ukumbi wa siasa ni kilimo Mkoani Iringa Agosti 12, 2021.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wakaguzi wa maeneo ya malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo yaliyofanyika  Agosti 12, 2021 kwenye ukumbi wa Siasa ni kilimo Mkoani Iringa.

 


Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji (wa tatu kutoka kulia), Bw. Peter Nyakigera akiwa kwenye picha ya pamoja na  wataalam wa Mifugo na wakaguzi kutoka ngazi za Wizara na Mikoa mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa maeneo ya malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo  kwenye ukumbi wa Siasa ni kilimo  Mkoani Iringa. (12/08/2021.)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni