Nav bar

Jumanne, 17 Agosti 2021

TADB YAOMBWA KUENDELEA KUWASAIDIA WAVUVI NCHINI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuwasaidia wavuvi  katika mambo matatu ikiwemo kuwaondoa wavuvi  kutoka kwenye uvuvi wa  maji ya ndani na kuwapeleka kuvua kwenye maji ya Kitaifa kwa kutumia maboti ya kisasa badala ya mitumbwi na ngalawa.

Ombi hilo lilitolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah alipokuwa akiongea na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania  (TADB) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Frank Mugeta,  alisema uvuvi wa samaki katika ukanda wa bahari unaweza kuongezeka iwapo wataweza kuwasaidia wavuvi katika mambo mbalimbali.

Pia, kuwaondoa wavuvi wadogo wadogo kutoka kwenye uvuvi wa  maji ya ndani na kuwapeleka kuvua kwenye maji ya Kitaifa kwa kutumia maboti ya kisasa badala ya mitumbwi na ngalawa ambazo wengi wao bado wanazitumia.

“Sasa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza kutekeleza baadhi ya mikakati kuwawezesha wafugaji samaki wadogo kwenye maji ya asili kukabilina na changamoto za uwekezaji mdogo  katika maeneo yao lakini hapo bado tuna changamoto,”alisema.

Alisema mafanikio katika utekelezaji wa mikakati yanategemea  kwa kiasi kikubwa  ushiriki wa Taasisi za kifedha za ndani pamoja na nje.

Alisema Wizara imeanzisha dawati la sekta binafsi ili kuratibu upatikanaji wa mikopo kwa vyama vya ushirika kwa kuyafanyia marekebisho maandiko yao ili yakidhi matakwa ya Kibenki.

“Kufikia Februari 2021, dawati limewezesha  kupokelewa  kwa maombi ya mikopo  ya uvuvi katika Benki ya TADB yenye thamani  ya shilingi bilioni 51.4 lakini kiasi kilichotolewa hadi sasa ni shilingi bilioni 1.2 kwa vyama vya ushirika vitatu  katika Wilaya ya Ukerewe, Buchosa na Chato,”alisema.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Mugeta amesema mara baada ya kikao hicho wataenda kuangalia namna ya kuisaidia sekta hiyo ambayo inaajiri watanzania wengi.

Alisema wataisaidia sekta hiyo kutokana na kufanyika kwa  tafiti nyingi ambazo zitawaongoza wao wasaidie sehemu zipi ili kuhakikisha Mtanzania anaweza kujikwamua kimaisha.

“Niahidi wataalam wetu watakaa,  hili ni eneo la kusapoti kwa nguvu zetu zote nimeteuliwa nina siku 10 bado nina nguvu hivyo tutapata majawabu ya haraka  ili tuone tunaanzia wapi.Tunataka kuhakikisha sekta ya uvuvi inaajiri watu wengi nafikiri ni eneo ambalo tutaliangalia kwa kina zaidi,”alisema.

Awali akitoa wasilisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi wa Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara hiyo, Dkt. Nazael Madalla alisema uvuvi ni miongoni mwa sekta zinazoajiri watu wengi wa kipato cha chini ambapo moja kwa moja takribani wavuvi na wakuzaji viumbe maji  wapatao 225,435.

Alisema zaidi ya watanzania milioni 4.5 wameendelea kupata kipato cha kila siku kutokana na shughuli zinazohusiana na sekta ya uvuvi ikiwemo kuunda na kutengeneza boti, kuuza na kushona nyavu kutengeneza na kuuza  barafu, biashara ya samaki na mazao yake.

Mkurugenzi huyo alisema sekta hiyo inachangia katika lishe na usalama wa chakula ambapo takribani asilimia 30 ya protein itokanayo na wanyama inachangiwa na samaki.

Alisema kwa upande wa kipato na fedha za kigeni katika mwaka 2020-2021 tani 483,756.4 zilivunwa na kuingiza kipato cha shilingi trilioni 2.42 kati ya mavuno hayo tani 41,319.00 na samaki hai wa mapambo 165,413 wenye thamani ya shilingi bilioni 18.91.

Mkurugenzi huyo amesema sekta hiyo ni muhimu kwani  inachangia pato la Taifa kwa asilimia 1.7

Alisema kwa sasa kiasi cha rasilimali za samaki  kwenye maji ni zaidi ya tani nne ambapo amedai kiasi kinachoweza kuvunwa  bila kuathiri mazingira ni tani 750,000.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akieleza lengo la kufanya kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Mugeta (hayupo pichani) ikiwa ni pamoja na kuomba kuwasaidia wavuvi kupata mikopo Ili kuweza kutatua changamoto zao katika masuala ya Uvuvi  kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Agosti 16, 2021.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Mugeta akielezea namna watakavyoweza kuiendeleza Sekta ya Uvuvi kwa kuwapatia wavuvi mkopo Ili waweze kujiendesha kwenye shughuli zao za Uvuvi  kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Agosti 16, 2021.

Mkurugenzi wa Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt Nazael Madalla, akiwasilisha mada wakati wa kikao na wajumbe kutoka Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Agosti 16, 2021.

Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatama, (waliokaa kulia) akiwa kwenye  picha ya pamoja mara baada ya kukutana na wajumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) lengo likiwa ni  kuwasaidia Wavuvi kukabiliana na changamoto za uwekezaji mdogo katika maeneo yao pamoja kuvipatia vyama vya ushirika vya uvuvi mikopo ili viweze kujiendesha kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni