Nav bar

Ijumaa, 9 Aprili 2021

WIZARA IZALISHE VIFARANGA WA SAMAKI KWA WINGI-RAIS SAMIA.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzalisha kwa wingi vifaranga wa samaki ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na fursa ya ufugaji wa samaki ambayo imeonekana kuvutia watu wengi kwa hivi sasa.

 

Mhe. Samia ameyasema hayo wakati akiwaapisha Makatibu wakuu wa Wizara na watendaji wa taasisi mbalimbali aliowateua hivi karibuni tukio lililofanyika leo (06.04.2021)  Ikulu ya Mkoa wa Dar-es-salaam ambapo ameitaja njia hiyo ya ufugaji wa samaki kama “bluu economy”  ya watu wa chini.

 

“Lakini pia tumeharibu sana mazingira ya bahari kiasi kwamba kupata samaki ni mpaka mvuvi afike maeneo ya bahari kuu hivyo tunaweza kuyatumia maeneo ya pembeni kuweka vizimba ili watu wengine waendelee na uchumi wao wa blue” Amesisitiza Mhe. Samia.

 

Kwa upande wa sekta ya Mifugo, Mhe. Samia amesema kuwa Wizara ina wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na  upatikanaji wa mbegu bora za Mifugo pamoja na kusimamia masoko ya wafugaji huku pia akiitaka  kusimamia ubora pindi wafugaji wanapochinja mifugo yao.

 

“Ukienda Arabuni wanataka  sana nyama kutoka Tanzania lakini kiwango wanachokitaka sio kiwango tunachozalisha kwa sababu uzalishaji wetu upo chini sana na “quality” yetu ipo chini sana” Ameongeza Mhe. Samia.

 

Mhe. Samia ameiagiza Wizara hiyo kuendelea kutoa mafunzo kwa wafugaji kuhusu njia bora na za kisasa za ufugaji ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya unenepeshaji wa mifugo kutoka hatua ya awali mpaka anapelekwa machinjioni na kuwataka wafugaji kote nchini kuachana na ufugaji wa zamani usio na tija.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah ni miongoni mwa Watendaji walioteuliwa hivi karibuni na kuapishwa leo kwenye hafla hiyo.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni