Nav bar

Ijumaa, 9 Aprili 2021

NDAKI AONGOZA MAPOKEZI YA ULEGA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki leo amewaongoza viongozi, watendaji na watumishi wa Wizara hiyo kumpokea Naibu Waziri wake Mhe. Abdallah Ulega tukio jioni ya leo  (01.04.2021) makao makuu ya Wizara yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.

 

Mara baada ya kumpokea Mhe. Ulega, Mhe. Mashimba alitumia fursa hiyo kumueleza malengo mbalimbali ambayo  Wizara hiyo ilipangiwa kuyatekeleza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanaondokana na umasikini na sekta hizo zitengeneze ajira za kutosha hasa ikizingatiwa kuwa ni sekta za uzalishaji.

 

“Karibu sana, bahati nzuri wewe ni mwenyeji hivyo nina uhakika tutaongeza tija katika kuhakikisha tunawavusha salama wafugaji na wavuvi na tunaongeza mchango wa kutosha kwenye pato la taifa kwa sababu mpaka sasa sekta hizi mbili mchango wake ni mdogo sana” Alisisitiza Mhe. Ndaki.

 

Huku akionekana mwenye furaha Mhe. Ulega aliwashukuru watendaji mbalimbali wa Wizara hiyo kwa salamu nyingi za pongezi walizomtumia tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo ambapo aliwaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika utendaji wao wa kila siku.

 

“Nimerudi nyumbani na kwa kweli nimefurahi sana, nataka niwahakikishie tu nimekuja hapa ili tushirikiane kwa pamoja kwa ajili ya kutekeleza malengo ambayo Mhe. Rais anayatarajia kupitia sekta za Mifugo na Uvuvi” Aliongeza Mhe. Ulega.

 

Mhe. Ulega ameahidi kumpa ushirikiano wa kutosha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki huku pia akiwa na matumaini kuwa ushirikiano wao utaleta tija kwenye sekta zote mbili za Mifugo na Uvuvi.

 

Akitoa maelezo ya Utangulizi, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel mbali na kumkaribisha Mhe. Ulega kwa mara nyingine tena wizarani hapo aliahidi kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wowote atakapohitajika kufanya hivyo na kumhakikishia kuwa watumishi wote wa sekta ya Mifugo wapo tayari kufanya hivyo pia.

 

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Mhe. Ulega pamoja na kuwa ni kiongozi, kwenye sekta ya uvuvi amekuwa mtaalam mwenzao na mara zote walishirikiana naye katika shughuli mbalimbali za sekta hiyo hivyo kurejea kwake kwao imekuwa ni kama bahati.

 

“Kwa kweli hata niliposikia unarejea tena kwa sababu hata wakati ule tulikuwa hatukutumii tu kama Waziri bali mtaalam wa sekta ya Uvuvi kwa hiyo tuna uhakika kurejea kwake kutasaidia shughuli za uvuvi kuendelea zaidi” Alihitimisha Dkt. Tamatamah.

 

Mhe. Ulega anarejea Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama Naibu Waziri wa Wizara hiyo kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya kumuapisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango jana (31.03.2021).


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kulia) na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Makatibu wakuu wa Wizara hiyo, Prof. Elisante Ole Gabriel anayeshughulikia sekta ya Mifugo (kushoto) na Dkt. Rashid Tamatamah anayeshughulikia sekta ya Uvuvi (kulia) wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha Mhe. Ulega Wizarani hapo tukio lililofanyika leo (01.04.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akifafanua malengo ambayo Wizara yake imepangiwa kuyatekeleza mbele ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega muda mfupi baada ya kumkaribisha wizarani hapo tukio lililofanyika leo (01.04.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega wakiwa wameshikana mikono kama ishara ya Mhe. Ndaki kumkaribisha Mhe. Ulega Wizarani hapo tukio lililofanyika leo (01.04.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akisaini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kukaribishwa na kuingia ofisini kwake leo makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma leo (01.04.2021)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni