Nav bar

Jumatano, 21 Aprili 2021

NDAKI AWATAKA WATUMISHI KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA

Na Mbaraka Kambona,

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujiepusha na vitendo vya rushwa huku akionya kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake.

 

Ndaki aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya Mifugo uliofanyika jijini Dodoma Aprili 20, 2021.

 

Akizungumza na Wajumbe wa baraza hilo, Ndaki aliwataka watumishi hao kuzingatia uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za serikali huku akisema siyo vyema kwa mtumishi wa umma kutajwatajwa kuhusika na matukio maovu yanayoharibu taswira ya serikali.

 

"Niwaombe watumishi wote mjiepusha na vitendo vinavyokwenda kinyume cha Sheria za nchi na taratibu za kazi, haipendezi kuona mtumishi wa umma anatajwatajwa kwenye kashfa za rushwa, hili siyo jambo jema hata kidogo, epukeni rushwa,”alisema Ndaki

 

Aliongeza kuwa watumishi ni muhimu wakaheshimiana na kuzingatia nidhamu ya kazi, wajiepushe na vitendo vya ubabe na kudharauliana huku akisema kuwa kila mtu katika kazi ana umuhimu wake.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Elisante Ole Gabriel alimuahidi Waziri Ndaki kuwa wamepokea maelekezo yake na watahakikisha wanayasimamia vizuri ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi.

 

Prof. Ole Gabriel aliongeza kuwa kupitia baraza hilo wataendelea kuboresha bajeti ya sekta ya mifugo ili waweze kuwanyanyua wafugaji waweze   kufanya ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa mazoea.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) wakati akifungua Mkutano wa baraza hilo ambapo aliwasisitiza Watumishi wa Wizara kuzingatia Uadilifu, nidhamu na kujiepusha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao. Mkutano huo ulifanyika  jijini Dodoma. (20.04.2021)


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiongea na Wajumbe wa baraza hilo wakati akitoa neno la shukrani kwa (Mgeni rasmi), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) katika  Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) uliofanyika jijini Dodoma. (20.04.2021)

Baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) wakifuatilia matukio katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) uliofanyika jijini Dodoma (20.04.2021)

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Flaxed Mushi (kulia) akifuatilia majadiliano katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) uliofanyika jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi, Rasilimali Watu, Josephine Temihango. (20.04.2021)


Mhasibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Veronica Kishala (kulia) akifurahia jambo wakati akiongea na Afisa Usafirishaji, Kennedy Laizer walipokutana katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) uliofanyika jijini Dodoma.  (20.04.2021)


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi, Idara ya Sera na Mipango, Amos Zephania walipokutana katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) uliofanyika jijini Dodoma. (20.04.2021)


Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) wakimsikiliza Mgeni rasmi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma. (20.04.2021)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni